Maandamano yafanyika Afrika Kusini kulaani kuachiwa Mzungu katili
Wananchi wa Afrika Kusini wamefanya maandamano kulalamikia hatua ya mahakama ya nchi hiyo kumuachia huru raia mbaguzi wa Poland aliyemuua mmoja wa viongozi waliokuwa wanapinga utawala wa zamani wa ubaguzi wa rangi (apartheid).
Mwishoni mwa mwezi uliopita, Mahakama ya Katiba ya Afrika Kusini ilimuachia huru Janusz Walus, raia mbaguzi wa Poland aliyekuwa akitumikia kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya kumuua Chris Hani, mmoja wa viongozi waliokuwa wanapambana na apartheid.
Moja ya mabango yaliyokuwa yamebebwa na waandamanaji hao mjini Cape Town lilikuwa na ujumbe usemao "Tunataka uchunguzi wa kina wa mauaji ya kigaidi ya Chris Hani.'
Mandla Mandela, mjukuu wa rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela ambaye alikuwa miongoni mwa waandamanaji hao amesema, "Chris alikuwa mtu wa karibu na babu yangu (Nelson Mandela), kuachiwa huru kwa muuaji wa shujaa wetu kunatonesha kidonda na kukumbusha matukio chungu yaliyofanyika enzi za apartheid."
Kadhalika chama cha Kikomunisti cha Afrika Kusini kimekosoa vikali uamuzi huo wa Mahakama ya Katiba wa kumuachia huru raia huyo wa Poland mwenye misimamo ya kibaguzi. Hani alikuwa kiongozi wa chama hicho ambacho kina ukuruba na chama tawala ANC.
Janusz Walus alihamia Afrika Kusini mwaka 1981 na alikuwa muungaji mkono mkubwa wa mfumo usio wa kibinadamu wa Apartheid. Alitekeleza ukatili huo mwaka 1993, kitendo ambacho nusra kiitumbukize Afrika Kusini katika vita vya ndani.
Raia huyo mbaguzi wa Poland alihukumiwa kunyongwa mwaka 1993, lakini hukumu hiyo iliangaliwa upya baadaye, na korti ya Afrika Kusini ikaamua kumfunga maisha jela.
Mfumo wa ubaguzi wa rangi wa Apartheid ambao ni miongoni mwa sura za ukatili na unyama wa kutisha na ubaguzi wa kizazi uliotawala Afrika Kusini kwa miaka mingi kwa maslahi ya wazungu waliowachache dhidi ya wazalendo weusi, ulifutwa rasmi nchini humo mwaka 1991.