Eritrea: Ethiopia imefanya hujuma ndani ya ardhi yetu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i9127-eritrea_ethiopia_imefanya_hujuma_ndani_ya_ardhi_yetu
Kwa mara nyingine tena Eritrea imeituhumu jirani yake Ethiopia kuwa imefanya mashambulizi ndani ya ardhi yake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 13, 2016 10:25 UTC
  • Eritrea: Ethiopia imefanya hujuma ndani ya ardhi yetu

Kwa mara nyingine tena Eritrea imeituhumu jirani yake Ethiopia kuwa imefanya mashambulizi ndani ya ardhi yake.

Taarifa ya Wizara ya Habari ya Eritrea imesema kuwa, harakati ya Tigrayan People's Liberation Front (TPLF) ambayo ni moja ya vyama vinne vinavyounda muungano unaotawala nchini Ethiopia ilifanya shambulio ndani ya ardhi ya Eritrea jana Jumapili. Hata hivyo taarifa hiyo haijabainisha taathira za shambulio hilo katika eneo la Tsorona lililoko katika mpaka wa nchi mbili hizo za Pembe ya Afrika. Hii ni katika hali ambayo, serikali ya Ethiopia haijatoa kauli rasmi kuhusiana na shambulio hilo ndani ya ardhi ya Eritrea. Nchi mbili hizi zimekuwa zikituhumiana kuwa kila upande unaunga mkono makundi ya waasi kwa lengo la kuangusha serikali zilizopo mamlakani.

Mwezi Septemba mwaka jana, Eritrea iliitahadharisha Ethiopia kuhusiana na hatua yake ya kuchochea vita na kuituhumu Addis Ababa kwamba inafanya njama za kutaka kuikalia kwa mabavu ardhi ya nchi hiyo.

Itakumbukwa kuwa, zaidi ya watu 70,000 waliuawa katika mapigano kati ya nchi mbili hizo za Pembe ya Afrika, katika kipindi cha miaka ya 1998 hadi 2000.