Waislamu wa Nigeria waandamana katika hauli ya mashahidi wa Zaria
Wananchi wa Nigeria wameandamana katika miji mbalimbali ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika katika hauli na kumbukumbu ya mashahidi waliouawa katika mauaji yaliyofanywa na vikosi vya usalama katika mji wa Zaria miaka saba iliyopita.
Taarifa zaiidi zinasema kuwa, Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Nigeria wameadhimisha kumbukumbu ya mwaka wa saba tangu yalipotokea mauaji ya kinyama yaliyofanywa na vyombo vya usalama vya Nigeria dhidi ya Waislamu katika mji wa Zaria.
Mbali na mji mkuu Abuja, miji mingine ya Nigeria imeshuhudia maandamano makubwa ya tukio hilo lililokuwa na umwagaji damu mkubwa ambapo waandamanaji walikuwa wamebeba picha za Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria.
Waandamanaji hao walikuwa na maberamu yaliyoandikwa jumbe mbalimbali kwa lugha ya Kihausa ambapo moja ya beramu hilo lililosomeka: Tunalaani mauaji ya mamia ya Waislamu wa madhehebu ya Shia katika mji wa Zaria yaliyofanywa na wanajeshi.
Katika shambulio hilo la Disemba 12, 2015, inakadiriwa wanachama zaidi ya 1,000 wa harakati ya Kiislamu ya Nigeria, aghalabu wakiwa ni Waislamu wa madhehebu ya Shia waliuawa kwa kufyatuliwa risasi na jeshi la Nigeria. Miongoni mwa waliouawa walikuwemo watoto watatu wa kiume wa Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria.
Katika siku iliyofuata, Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe Malama Zeenat walitiwa nguvuni wakati wanajeshi wa Nigeria walipovamia Husseiniyah ya Baqiyatullah na nyumba ya mwanazuoni huyo katika mji wa Zaria.