Ethiopia yatuma ujumbe Tigray kwa ajili ya kutekeleza mapatano ya amani
(last modified Tue, 27 Dec 2022 02:31:07 GMT )
Dec 27, 2022 02:31 UTC
  • Ethiopia yatuma ujumbe Tigray kwa ajili ya kutekeleza mapatano ya amani

Ujumbe wa ngazi ya juu wa timu ya serikali ya Ethiopia umeelekea Tigray kaskazini mwa nchi hiyo kwa ajili ya mazungumzo ya kutekeleza makubaliano ya amani ili kuhitimisha mzozo wa miaka miwili kati ya serikali ya Addis Ababa na Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF).

Serikali ya Addis Ababa na waasi wa TPLF wamekubaliana kuunda bodi ya pamoja ya usimamizi ya kuhakikisha kuwa mapatano ya amani yaliyofikiwa mwezi Novemba yanaheshimiwa na pande zote. Mapatano hayo yalifikiwa kwa shabaha ya kuhitimisha vita kandamizi huko Tigray. 

Miongoni mwa masharti ya mapatano hayo ni kipengele cha kuanzisha utaratibu wa ufuatiliaji wa masuala yaliyofikiwa, na pande mbili kufungamana na mapatano  hayo ili  kuwa na uhakika kwamba mapatano hayo yanatekelezwa na kupatiwa ufumbuzi aina yoyote ya ukiukaji utakaoshuhudiwa.

Maelfu ya makumi ya watu wameuawa katika miaka miwili ya umwagaji damu katika eneo la Tigray, kaskazini mwa Ethiopia. 

Taarifa ya serikali ya Ethiopia imeeleza kuwa, ujumbe huo ni wa kwanza wa ngazi ya juu wa serikali kuelekea huko Mekele katika kipindi cha miaka miwili. Ujumbe huo unaongozwa na Tagesse Chafo, Spika wa Bunge la Ethiopia.  

Hafla ya utiaji saini mapatano ya amani 

Mapatano ya amani kati ya serikali ya Ethiopia na harakati ya TPLF  yanatoa mwanya wa kupokonywa silaha vikosi vya waasi, kuanzishwa upya kwa mamlaka ya shirikisho huko Tigray na kufunguliwa tena njia za kupeleka misaada katika eneo la Tigray.