Ajali mbili za barabarani zaua watu 21 Nigeria
Dec 28, 2022 08:02 UTC
Polisi ya Nigeria imetangaza kuwa, watu 21 wamefariki dunia kutokana na ajali mbili za barabarani zilizotokea nchini humo siku ya Jumatatu na Jumanne.
Kuwar Tsukwam, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani cha Serikali ya Shirikisho katika jimbo la Niger, (FRSC) ameeleza katika taarifa kwamba, ajali ya kwanza ilitokea Jumatatu katikati ya eneo la kaskazini mwa nchi, ambapo magari mawili yaligongana uso kwa uso baada ya kupoteza udhibiti.
Kwa mujibu wa Tsukwam, watu 11 walifariki katika ajali hiyo iliyosababishwa na mwendo wa kasi wa magari hayo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na msemaji wa makao makuu ya FRSC Bisi Kazeem, ajali ya pili ilitokea jana Jumanne kwenye barabara kuu iliyoko kusini-magharibi mwa nchi, na kuua watu 10 na kujeruhi wengine sita, baada ya basi moja la kibiashara kutumbukia kwenye mtaro wa barabara wakati likijaribu kulikwepa lori lililokuwa likiendeshwa mkabala na njia ya trafiki.
Ajali mbaya za barabarani huripotiwa mara kwa mara nchini Nigeria; na mara nyingi husababishwa na upakiaji kupita kiasi, hali mbaya ya barabara na uzembe wa madereva katika uendeshaji.../
Tags