Libya: Hatuhitaji misaada ya nchi ajinabi kupambana na Daesh
Naibu Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya amesema kuwa nchi hiyo haihitaji misaada ya nchi ajinabi kwa ajili ya kuendesha vita dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh nchini humo.
Musa al Koni, Naibu Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya amesisitiza kuwa takwa pekee la serikali ya Libya kwa nchi za ulimwengu ni kupatiwa taarifa za kijasusi kupitia satalaiti ili kuweza kuwaangamiza magaidi wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh walioko nchini humo.
Musa al Koni amesema kuwa kundi la kigaidi la Daesh limewafanya wananchi wa Libya wawe kitu kimoja na kwamba wanazo silaha za kutosha kuendeshea mapambano dhidi ya Daesh, hata hivyo amesema Libya inahitaji misaada ya kibinadamu pia kwa ajili ya raia wake kama dawa na bidhaa za chakula.
Hii ni katika hali ambayo Fayez al Sarraj, Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya jana alisema kuwa upo ulazima wa kuendelezwa mapambano ya kuukomboa mji wa Sirte kutoka kwa magaidi wa Daesh na amewatolea wito raia wa nchi hiyo kuliunga mkono jeshi katika mapambano yake. Jeshi la Libya siku kadhaa zilizopita lilipiga hatua kubwa katika mapambano dhidi ya Daesh katika mji wa Sirte ambao unashikiliwa na kundi hilo tangu mwezi Juni mwaka jana. Mji wa Sirte unatambulika kama ngome muhimu ya Daesh huko Libya baada ya maeneo mengine yaliyovamiwa na kushikiliwa na kundi hilo huko Iraq na Syria.