UN yatiwa wasiwasi na mapigano ya mpakani kati ya Ethiopia na Eritrea
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema anatiwa wasiwasi na mapigano ya mpakani kati ya Ethiopia na Eritrea.
Ban Ki-moon jana alikutana na kufanya mazungumzo huko Brussels mji mkuu wa Ubelgiji na Hailemariam Desalegn, Waziri Mkuu wa Ethiopia na kuzitolea wito serikali za nchi hiyo na jirani yake Eritrea kufanya mazungumzo. Ban Ki-moon amezitaka Addis Ababa na Asmara kujiepusha na hatua zozote zinazoshadidisha hali ya mivutano kati ya nchi mbili hizo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesistiza kuwa Ethiopia na Eritrea zinapasa kutatua hitilafu zao kwa njia ya amani na kutekeleza makuballiano ya amani yaliyosainiwa na nchi mbili hizo mwaka 2000. Mapigano makali yalijiri siku kadhaa zilizopita na kusababisha vifo vya watu wengi kutoka pande zote mbili katika mipaka ya nchi mbili hizo; hata hivyo hadi sasa hakujatolewa idadi sahihi ya waliouliwa na kujeruhiwa. Serikali ya Ethiopia imeyataja mapigano hayo kuwa ni mapigano makali zaidi kuwahi kujiri katika miaka ya hivi karibuni kati yake na Eritrea. Kabla ya mapigano hayo ya majuzi, itakumbukwa kuwa Ethiopia na Eritrea zilikuwa zikizozana kuhusu suala la mpaka kuanzia mwaka 1998 hadi 2000.