Mjukuu wa Mandela atumia mashindano ya CHAN kutangaza kupigania ukombozi wa Palestina
Mjukuu wa shujaa wa ukombozi, Nelson Mandela amesisitizia ulazima wa kupigania ukombozi wa Palestina na kupaza sauti za kuungwa mkono taifa hilo madhlumu.
Shirika la habari la FARS limeripoti habari hiyo jana Jumapili na kumnukuu Zwelivelile Mandela akisema hayo katika Uwanjwa wa Michezo wa Nelson Mandela nchini Algeria katika kilele cha sherehe za ufunguzi wa Kombe la Mataifa ya Afrika huku akishangiriwa kwa sauti kubwa na wapenzi wa ukombozi wa Palestina waliofurika uwanjani hapo.
Nalo toleo la mtandaoni la gazeti la "Rai Elyoum" limeandika kwamba, moja ya matukio muhimu ya ufunguzi wa michuano hiyo ni kushiriki Zwelivelile Mandela, mjukuu wa Nelson Mandela, katika uwanja uliopewa jina la babu yake. Wakati wa hotuba yake, Zwelivelile Mandela alitumia kaulimbiu ya uhuru wa Palestina kutoka baharini hadi mtoni.
Alisema: Uhuru wetu haujakamilika bila uhuru wa Palestina. Kwa hiyo, sote tunasimama pamoja kupigania ukombozi wa Palestina."
Ikumbukwe kuwa, moja ya matukio yenye kuvutia katika mashindano ya Soka ya Kombe la Dunia ya mara hii huko Qatar ni kitendo cha watazamaji kutoka nchi mbalimbali kuiunga mkono Palestina mkabala wa utawala wa Kizayuni.
Katika Mashindano hayo dunia ya Soka mwaka jana wa 2022 huko Qatar, watazamaji wa nchi mbalimbali na hasa wa nchi za Kiarabu walikataa kuhojiwa na vyombo vya habari na maripota wa Israel na walikuwa wakionyesha uungaji mkono wao kwa Palestina wakati mechi mbalimbali zikifanyika.