Iran yazindua makombora ya kisasa ya 'Nasr'
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i934-iran_yazindua_makombora_ya_kisasa_ya_'nasr'
Wizara ya Ulinzi ya Iran imelikabidhi Jeshi la Anga la Jamhuri ya Kiislamu shehena ya kwanza ya makombora ya kisasa ya anga yakulikanayo kwa jina la 'Nasr' au Ushindi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 09, 2016 23:53 UTC
  • makombora ya Iran
    makombora ya Iran

Wizara ya Ulinzi ya Iran imelikabidhi Jeshi la Anga la Jamhuri ya Kiislamu shehena ya kwanza ya makombora ya kisasa ya anga yakulikanayo kwa jina la 'Nasr' au Ushindi.

Akiongea katika hafla ya uzinduzi wa makombora hayo jana Jumanne, Waziri wa Ulinzi wa Iran, Brigedia Jenerali Hussein Dehqan amesema makomboa ya Nasr yametengezwa kwa utaalamu wa hali ya juu wa kulenga shabaha bila kukosea na kwamba yanaweza kuvurumishwa kutoka kwenye ndege yoyote ya kivita. Mbali na Dehqan, hafla hiyo imehudhuriwa na Brigedia Jenerali Hassan Shah Safi, Mkuu wa Jeshi la Anga la Iran.

Brigedia Jenerali Dehqan amesema Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kuimarisha uwezo wake wa kiulinzi na kiusalama ili kuzima chokochoko za maadui wa nchi hii. Agosti 25 mwaka jana, wataalamu wa Iran walizindua uzalishaji wa makombora ya Nasr.

Waziri wa Ulinzi wa Iran amesisitiza kuwa, taifa hili halibabaishwi na vitisho vyovyote na kwamba hakuna chochote kinachoweza kulizuia kuimarisha uwezo wa kuwalinda wananchi wake.

Iran imekuwa ikikariri kuwa, kuzidi kuimarisha uwezo wake wa kijeshi sio kwa ajili ya kuzitishia nchi za eneo hili, bali ni kwa lengo la kulihami taifa kutokana na chokochoko za maadui.