Botswana yatishia kukata uhusiano na kampuni ya almasi ya Uingereza
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i94000-botswana_yatishia_kukata_uhusiano_na_kampuni_ya_almasi_ya_uingereza
Rais Mokgweetsi Masisi wa Botswana ameonya kuwa, huenda nchi yake ikavunja uhusiano na shirika kubwa la kimataifa la almasi la De Beers, lenye makao yake huko London, Uingereza, kwa kupunjwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 13, 2023 06:47 UTC
  • Botswana yatishia kukata uhusiano na kampuni ya almasi ya Uingereza

Rais Mokgweetsi Masisi wa Botswana ameonya kuwa, huenda nchi yake ikavunja uhusiano na shirika kubwa la kimataifa la almasi la De Beers, lenye makao yake huko London, Uingereza, kwa kupunjwa.

Rais wa Botswana alitoa indhari hiyo jana Jumapili na kufafanua kuwa, iwapo mazungumzo ya kujadidisha mapatano kati ya nchi hiyo na shirika la De Beers hayatakuwa na maslahi kwa taifa hilo, basi nchi hiyo ya kusini mwa Afrika itavunja uhusiano na kampuni hiyo ya Uingereza.

Makubaliano baina ya pande mbili hizo kwa anwani ya Debswana, yalitiwa saini mwaka 2011, na yalitazamiwa kumalizika 2021. Hata hivyo muda wake ulirefushwa hadi Juni 30 mwaka huu 2023, kutokana na janga la Corona.

Akihutubia mkutano wa chama tawala cha Botswana Democratic Party (BDP) hiyo jana katika kijiji chake cha Moshupa, yapata kilomita 65 kutoka Gaborone, mji mkuu wa Botswana, Rais Masisi alisema, 'Iwapo hatutafikia mapatano yenye maslahi kwa pande zote mbili, kila upande utalazimika kufungasha virago na kuondoka."

Kwa mujibu wa makubaliano ya 2011, shirika la De Beers liliuza asilimia 90 ya almasi ya Botswana, huku nchi hiyo ya Kiafrika ikipiga mnada asilimia 10 iliyosalia ya madini hayo yenye thamani kupitia kampuni ya almasi ya  Okavango. Hata hivyo hisa ya Botswana iliongezeka hadi asilimia 25 mwaka 2020.

Madini ya almasi

Rais wa Botswana amebainisha kuwa,"Hivi sasa tuna ufahamu mkubwa juu ya soko la almasi, na tumegundua kuwa almasi yetu inatengeza faida kubwa, lakini tumekuwa tukipokea fedha chache kuliko inavyostahiki." 

Alipoingia madarakani mwaka 2018, Rais Mokgweetsi Masisi aliahidi kuiondoa nchi hiyo katika utegemezi wa almasi. Botswana ambayo ina jamii ya watu milioni mbili na laki tano, ina kiwango cha watu wasio na ajira cha asilimia 20 haswa vijana.

Wanaharakati barani Afrika wamekuwa wakilalamikia jinai za utawala wa kikoloni wa Uingereza katika nchi za bara hilo, ambapo utajiri mkubwa ulioporwa barani humo ulitajirisha familia ya kifalme ya mkoloni huyo mkongwe. UK inaedelea kupora utajiri wa Afrika kupitia ukoloni mamboleo.