Mwanasoka wa Ghana ni miongoni mwa waliofariki katika mitetemeko ya ardhi Uturuki
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i94214-mwanasoka_wa_ghana_ni_miongoni_mwa_waliofariki_katika_mitetemeko_ya_ardhi_uturuki
Mwanasoka mashuhuri wa Ghana Christian Atsu ni miongoni mwa makumi ya maelfu ya watu waliofariki kufuatia mitetemeko miwili mikubwa ya ardhi nchini Uturuki.
(last modified 2026-01-14T11:42:18+00:00 )
Feb 19, 2023 06:30 UTC
  • Mwanasoka wa Ghana ni miongoni mwa waliofariki katika mitetemeko ya ardhi Uturuki

Mwanasoka mashuhuri wa Ghana Christian Atsu ni miongoni mwa makumi ya maelfu ya watu waliofariki kufuatia mitetemeko miwili mikubwa ya ardhi nchini Uturuki.

Wakala wa Uturuki wa mwanasoka huyo maarufu kutoka Ghana aliyewahi kuichezea timu ya Chelsea amesema kwamba amepatikana akiwa amekufa chini ya vifusi vya jengo lililoporomoka kusini mwa Utruki kufutia mitetemeko ya ardhi hivi karibuni nchini humo.

Murat Uzunmehmet amewaambia wanahabari mjini Hatay ambako mwili wake ulipatikana, kwamba baadhi ya vitu vyake pia vimepatikana, ikiwemo simu yake. Taarifa zinasema Atsu alikuwa aondoke kusini mwa Uturuki saa chache kabla ya kutokea tetemeko hilo lakini akaamua kubaki kidogo pamoja na wachezaji wenzake baada ya kupata goli la ushindi kwenye mechi ya Super Lig hapo Februari 5.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Ghana imesema kwamba ndugu yake pamoja na dada yake pacha walikuwepo wakati mwili huo ukigunduliwa. Ubalozi wa Ghana unaendelea na mipango za kuurejesha nyumbani kwa ajili ya mazishi.

Nyumba iliyoporomoka katika zilzala Uturuki

Atsu alihamia Uturuki baada ya kucheza katika vilabu tisa tofauti katika nchi nyingine tano. Aliingia katika klabu ya FC Porto ya Ureno akiwa winga kijana, kisha akasajiliwa na Chelsea nchini Uingereza. Baadaye alikaa kwa misimu mitano Newcastle United kuanzia 2016-2021.

Habari za kifo chake, ambazo zilithibitishwa na wawakilishi wake, zilizua huzuni katika klabu hizo, miongoni mwa wachezaji wenzake wa zamani, na katika soka la kimataifa.

Hadi sasa watu zaidi ya 46,000 wamepoteza maisha katika mitetemeko miwili mikubwa ya ardhi iliyozikumba Uturuki na Syria mnamo Februari 6, 2023.