ICC: Tunafuatilia karibu matukio ya kisiasa nchini Kenya
Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) imesema inafuatilia kwa karibu matukio ya kisiasa yanayojiri hivi sasa nchini Kenya na imetoa indhari kuwa haitachelea kufungua kesi mpya dhidi ya watenda jinai iwapo nchi hiyo itatumbukia tena katika machafuko ya baada ya uchaguzi kama ya mwaka 2007/2008.
Akiongea kwa mara kwanza tangu kusambaratika kwa kesi zilizokuwa zikiwakabili Wakenya sita katika mahakama ya ICC, Fatou Bensouda, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa mahakama hiyo yenye makao makuu yake mjini Hague nchini Uholanzi amesema chombo hicho cha kimataifa kitawawajibisha wale wote watakaohusika na kuchochea ghasia wakati na baada ya uchaguzi mkuu mwaka ujao 2017. Amesema kuwa: "Mimi siombi mabaya yafanyike nchini Kenya, tahadhari yangu ni kwa wale watakaozusha ghasia nchini humo na kukiuka haki za msingi sawia na kutenda jinai dhidi ya binadamu wakati na baada ya uchaguzi huo."
Kauli ya Bensouda imetolewa sambamba na kuachiwa huru kwa dhamana, wanasiasa wanane waliokamatwa na kuwekwa korokoroni kwa muda siku nne, kwa tuhuma za uchochezi. Wanasiasa hao wanajumuisha wabunge na maseneta kutoka upande wa serikali na kambi ya upinzani.
Mapema mwezi Aprili mwaka huu, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ilitangaza kuwa Naibu wa Rais wa Kenya William Ruto na mwanahabari Joshua Sang hawakuwa na kesi ya kujibu kufuatia kuvurugika mkondo wa kesi dhidi yao. Mwezi Machi mwaka 2015 ICC pia ilitupilia mbali kesi kama hiyo dhidi ya Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta. Kabla ya hapo mahakama hiyo pia ilifuta kesi kama hiyo ya mwanasiasa maarufu wa Kenya, Henry Kosgei Septemba 2011 huku kesi dhidi ya aliyekuwa kamishna wa polisi ya Kenya Hussein Ali ikitupiliwa mbali Januari 2012.