Mamia ya wahajiri wa Kiafrika warejea nyumbani wakitokea Tunisia
(last modified Sun, 05 Mar 2023 10:39:12 GMT )
Mar 05, 2023 10:39 UTC
  • Mamia ya wahajiri wa Kiafrika warejea nyumbani wakitokea Tunisia

Mamia ya wahajiri wa Kiafrika wamerejea katika nchi zao wakitokea Tunisia, siku chache baada ya Rais Kais Saied wa nchi hiyo kutoa matamshi yaliyoonekana kuwa dhidi ya wahamiaji nchini humo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, wahajiri takriban 300 jana Jumamosi waliwasili katika nchi zao za Mali na Ivory Coast wakitokea Tunisia, wakihofia kuibuka wimbi la mashambulizi ya kibaguzi kufuatia matamshi ya kutatanisha ya hivi karibuni ya Rais Kais Saied.

AFP imesema raia 135 wa Mali wakiwemo wanaume 97, wanawake 25 na watoto 13 waliwasili Bamako jana jioni na kupokewa na Waziri wa Ulinzi wa Mali, Sadio Camara na mwenzake anayeshughulikia masuala ya Wamali walioko ughaibuni, Alhamdou Ag Ilyene.

Ndege nyingine iliyokuwa imebeba wahajiri 145 wa Ivory Coast iliwasili Abidjan jana jioni, ambapo wahamiaji hao walipokewa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Patrick Achi na mawaziri wengine kadhaa. Kundi la kwanza la wahamiaji 50 raia wa Guinea liliondoka Tunisia Jumatano iliyopita.

Mwezi uliopita, Rais Kais Saied wa Tunisia alizungumzia wimbi la wahamiaji haramu kutoka nchi za Afrika za kusini mwa Jangwa la Sahara na kuhimiza kukabiliana na wimbi hilo. Saied alisisitiza kuwa, hali ya hivi sasa "si ya kawaida," na alitoa mwito wa kuchukuliwa hatua kali za kukomesha wimbi hilo.

Maelfu waliandamana Tunisia Jumamosi kulaani kuzorota kwa hali ya kiuchumi 

Umoja wa Afrika ulitoa taarifa ya kueleza kusikitishwa kwake na kushangazwa na matamshi hayo ya 'kibaguzi' ya Rais wa Tunisia. Hata hivyo siku chache zilizopita, serikali ya Tunisia ilikanusha madai kuwa imewafukuza kwa nguvu wahamiaji kutoka nchi za Afrika za kusini mwa Jangwa la Sahara.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Tunisia ilisema: "Baada ya kuenea madai ya kulazimishwa kuondoka baadhi ya wahamiaji kutoka nchi ndugu za Afrika za kusini mwa Jangwa la Sahara, tunathibitisha kwamba hakuna raia hata mmoja wa nchi hizo aliyefukuzwa kwa nguvu; lakini kumesajiliwa baadhi ya maombi ya kurejea kwa khiari wakaazi wasio na kibali nchini Tunisia.