Tunisia yaijia juu polisi ya Ufaransa kwa kuua raia wake Marseille
Tunisia imewasilisha malalamiko rasmi kwa Ufaransa, ikilaani mauaji ya raia wa nchi hiyo ya Kiarabu yaliyofanywa na polisi wa Ufaransa katika mji wa kusini wa Marseille.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Tunisia imesema katika taarifa yake kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook kuwa, "Kufuatia mauaji ya raia wa Tunisia, Abdelkader Dhibi mnamo Septemba 2, 2025 huko Marseille, na kwa maagizo ya Mheshimiwa Rais wa Tunisia, Katibu wa Waziri wa Mambo ya Nje, Uhamiaji na Watunisia Waishio Nje ya Nchi alimuita alasiri ya leo (jana Jumatano) Septemba 3, Balozi Mdogo wa Ufaransa nchini Tunisia, kutokana na kutokuwepo Balozi wa Jamhuri ya Ufaransa ambaye yuko nje ya nchi, kumwarifu kuhusu malalamiko makali (ya Tunis) dhidi ya mauaji (hayo) yaliyofanywa na maafisa wa polisi wa Ufaransa."
"Waziri wa Mambo ya Nje amemtaka Balozi Mdogo wa Ufaransa kuifahamisha serikali ya nchi yake kwamba, Tunisia inachukulia tukio hilo kama mauaji yasiyohalalishika, na inatarajia Ufaransa itachunguza mauaji hayo kwa kina haraka iwezekanavyo, na kuwabebesha dhima (wahusika)," imeongeza taarifa hiyo.
Wizara hiyo imeeleza kuwa, Tunisia "imeazimia kuchukua hatua zote kulinda haki za marehemu na familia yake." Rais wa Tunisia Kais Saied "alimwagiza Balozi wa Tunisia huko Paris kuwasilisha malalamiko hayo ya Tunis kwa mamlaka za Ufaransa na kuchukua hatua zinazohitajika kwa uratibu na Naibu Balozi wetu huko Marseille, ili kuharakisha uhamisho wa mwili wa marehemu kwenda Tunisia haraka iwezekanavyo."
Vyombo vya habari vya Ufaransa vilidai Jumanne kwamba, "Abdelkader aliuawa na maafisa wa polisi wa Ufaransa katikati mwa Marseille eti baada ya kuwachoma kisu watu watano."
Vyanzo hivyo vilidai kuwa kijana huyo wa Tunisia, ambaye alikuwa akiishi kihalali nchini Ufaransa, aligombana na watu sokoni kabla ya kukimbizwa na vijana kuelekea Old Port, ambapo polisi wa Ufaransa walimpiga risasi.