Mar 14, 2023 07:53 UTC
  • Kimbunga cha Freddy chaua watu wasiopungua 100 huko Malawi

Msumbiji na Malawi zinatathmini maafa ya Kimbunga kwa jina la Freddy, ambacho kimelikumba eneo la Kusini mwa Afrika kwa mara ya pili katika kipindi cha mwezi mmoja sasa na kusababisha uharibifu mkubwa na kuua watu wasiopungua 100 huko Malawi.

Kimbunga Freddy ni moja ya vimbunga vikali kuwahi kuripotiwa katika ukanda wa kusini wa dunia na kinaweza kuwa kimbunga cha kitropiki cha muda mrefu zaidi. Haya yameripotiwa na a Shirika la Hali ya Hewa Duniani.

Jumamosi iliyopita kimbunga hicho kiliezua mabati ya majengo na nyumba kadhaa na kusababisha kuenea mafuriko katika bandari ya Quelimane kabla ya kuelekea katika maeneo mengine huko Malawi sambamba na kunyesha mvua kubwa zilizosababisha maporomoko ya udongo. 

Polisi nchini Malawi wameeleza kuwa kimbunga cha Freddy kimeuwa  watu wasiopungua 99  nchini humo; watu 85 wakiaga dunia  katika mji wa Blantyre kusini mwa nchi hiyo; ambako mvua kubwa zimesababisha mafuriko. 

Polisi nchini Malawi wanaendelea kuwatafuta watu huko Chilobwe na Ndirande; maeneo ambayo ni miongoni mwa yale yaliyoathirika sana na mafuriko huko Blantyre. Jana Jumatatu mvua ziliendelea kunyesha katika maeneo hayo huku wakazi wake wengi wakisalia bila ya huduma ya umeme. 

Watu wasiopungua wanne pia wamepoteza maisha huko Msumbiji. Kiwango kamili cha uharibifu na watu waliopoteza maisha huko Msumbiji hadi sasa bado hakijabainika, kwani umeme na  mawasiliano ya simu yalikatika katika baadhi ya maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko. 

Tags