Kushadidi madhara ya vita na vikwazo kwa mataifa masikini
Migogoro wa kisiasa na kiuchumi hususan vita ni mambo ambayo kwa hakika yamekuwa na taathira hasi kwa hali ya uchumi wa mataifa masikini hususan nchi za Kiafrika.
Hali imekuwa mbaya zaidi kiasi kwamba, aktharui ya mataifa hayo yamedhurika mno na vita vya Ukraine na hata maisha ya raia wake kuwa hatarini.
Katika uwanja huo, Muhammad al-Ghazali al-Tijani Siraj, balozi wa Sudan huko Moscow Russia anasema: Vikwazo sio hatua athirifu na mwafaka kwa ajili ya kupatia ufumbuzi matatizo na hata kuhusiana na mikataba ya nafaka au usafirishaji wa mbolea kwa mataifa yenye uhitaji na kueleza kwamba, vikwazo havijawa na taathira hasi kwa Russia pekee bali hata kwa mataifa masikini na yenye uhitaji.
Balozi wa Sudan nchini Russia ameashiria nukta hii kwamba, watu dhaifu kabisa kutokana na mazingira ya kijiografia wanaishi katika mataifa masikini ya Afrika na Asia na kutokuweko himaya na uungaji mkono wa daima kwa sekta ya nafaka kunaweza kuwa na taathira ya moja kwa moja kwa usalama wa chakula wa nchi hizo. Aidha amesema, vikwazo vya Magharibi dhidi ya Russia vinatoa pigo kwa nchi masikini.

Licha ya kuchukua wigo mpana vita vya Russia na kuzishughulisha nchi nyingi za dunia na mgogoro wa kiuchumi, lakini nchi za Kiafrika ndizo ambazo zaidi zimekumbwa na hali ya kutengwa kiasi kwamba, akthari ya nchi hizo zinakabiliwa na tatizo la kujidhaminia chakula na dawa. Hali imekuwa mbaya kiasi kwamba, Rais Macky Sall wa Senegal alitahadharisha hivi karibuni kuhusiana na mahitaji ya nafaka kwa nchi masikini barani Afrika.
Kuendelea vita vya Ukraine kumezifanya nchi nyingi za Kiafrika kukabiliwa na hali ngumu sana. Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa ni kuwa, vita nchini Ukraine vimepelekea kupanda kwa bei ya vyakula na nafaka katika maeneo mbalimbali duniani na kufikia katika kiiwango cha juu kabisa. Hali hiyo ni mbaya zaidi barani Afrika, kwani akthari ya mataifa hayo yanaagiza vyakula na nafaka kutoka nje huku yakiwa na uchumi dhaifu.
Takwimu zinaonyesha kuwa, takribani watu bilioni moja na milioni 700 ulimwenguni ambapo akthari yao wanaishi barani Afrika wanakabiliwa na hatari ya uhaba wa chakula. Kadhalika zaidi ya mataifa 36 yamepata pigo kubwa kutokana na kutegemea kudhamini na kuingiza ngano kutoka nchini Russia na Ukraine.
Hii ni katika hali ambayo, nchi za Kiafrika hususan katika miaka ya hivi karibuni kutokana na sababu mbalimbali kama mabadiliko ya tabianchi, kuongezeka idadi ya watu, kushadidi ukosefu wa usalama unaosababishwa na kuenea makundi ya kigaidi, maradhi ya Covid-19 yaliyoukumba ulimwengu mzima na taathira zake hasi ni mambo ambayo yanatajwa na wajuzi wa mambo kuwa, yamechangia pakubwa katika kuzipa changamto nchi hizo katika kujidhaminia chakula, dawa na suhula muhimu za kitiba. Hivi sasa kutokana na kukatwa usafirishaji wa ngano barani Afrika kufuatia vita vya Ukraine sambamba na kusitishwa misaada ya baadhi ya mataifa na asasi za kimataifa, njaa, umasikini na ukosefu wa ajira ni mambo ambayo yameshadidi na kuongezeka mno.

Licha ya kuwa kumefanyikka mazunguumzo na hata kufikiwa makubaliano na Russia kwamba, mwenendo wa Russia kusafirisha ngano kuelekea barani Afrika uanze tena, lakini utendaji wa madola ya Magharibi na kuibiwa shehena za ngano ni mambo ambayo kivitendo yamepelekea Moscow kusitisha hilo au kufanyika kwa sura ya kuchelewa sana.
Vasily Nabenzya, balozi na mwakilishi wa kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa anasema: Kutowasili nafaka ya Ukraine kwa nchi zilizoko katika hali ya kustawi na mataiifa ya Kiafrika yaliyokumbwa na ukame niijambo linalokinzana na jukumu lililoainishwa katika makubaliano ya kusafirisha nafaka.
Katika miongo ya hivi karibuni nchi nyingi za Kiafrika ambazo ziliandaa mindomsingi ya kiuchumi zikilenga kuboresha na kustawisha hali zao za kiuchumi zimekumbwa na kigingi kigumu na kuwa wahanga wakuu wa matukio ya sasa ya dunia. Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) umesema katika ripoti yake ya hivi karibuni kabisa kwamba: Nchi za Kiafrika mwaka jana zilikuwa na matumaini ya kushuhudia kuhuika uchumi wao, lakini ghafla moja kukaibuka vita vya Ukraine na sababu nyingine mbalimbali kama janga la Corona ambalo limetikisa uchumi wa dunia. Hali hii imeyafanya mataifa haya ya Kiafrika kuwa wahanga wakuu wa matukio yasiyotarajiwa ya dunia kiasi kwamba, kunatabiriwa kupungua ustawi wa kiuchumi katika eneo la nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara na kufikia asilimia 3.6.
Hivi sasa balozi wa Sudan nchini Russia na mataifa mengine ya Kiafrika yametahadharisha na kutoa mwito wa nchi hizo kuzingatiwa zaidi. Inavyoonekana ni kuwa, mataifa masikini ya Kiafrika yamekuwa wahanga wakubwa wa vita na vikwazo vya madola ya Magharibi.