Msemaji wa Serikali ya Iran: Uuzaji nje mafuta hauwezi kusitishwa
(last modified Sat, 15 Mar 2025 12:36:39 GMT )
Mar 15, 2025 12:36 UTC
  • Msemaji wa Serikali ya Iran: Uuzaji nje mafuta hauwezi kusitishwa

Msemaji wa Serikali ya Iran amesisitiza kuwa uuzaji nje mafuta wa Iran hauwezi kusimamishwa na hakukuwa na haja ya kuwekwa vikwazo vipya iwapo vile vya huko nyuma vilikuwa na taathira.

Fatimeh Muhajirani ameeleza haya akijibu hatua ya Marekani ya kumuwekea vikwazo Waziri wa Mafuta wa Iran. 

mapema leo Jumamosi, Muhajirani ametuma ujumbe katika ukurasa wake wa X akisema kwamba: Wanapomwekea vikwazo kwa kasi Bwana Pak Nejad inamaanisha kuwa wana wasiwasi kuhusu shughuli na hatua zinazotekelezwa na Wizara ya Mafuta. 

Msemaji wa Serikali ya Iran amesema: Tehran haiwezi kusimamisha kuuza nje mafuta yake; na sehemu ya Iran katika soko la kimataifa imelindwa. 

Wizara ya Fedha ya Marekani, siku ya Alhamisi Machi 13 ilitoa taarifa na kutangaza kuwa, Idara ya Udhibiti wa Mali za Kigeni (OFAC) imemuwekea vikwazo Mohsen Pak Nejad, Waziri wa Mafuta wa Iran ambaye anasimamia uuzaji nje wa mafuta ya Iran yenye thamani ya mabilioni ya dola. 

Mohsen Pak Nejad

Kufuatia vikwazo hivyo, Wizara ya Mafuta ya Iran imetoa taarifa na kusema: Vikwazo alivyowekea Mohsen Pak Nejad kutokana na jitihada zake kubwa za kuuza nje mafuta ya Iran ni hatua mpya zaidi katika fremu ya mashinikizo ya kiwango cha juu ya Marekani; na vikwazo hivi  vimewekwa huku wizara anayoiongoza ikiwa hata haijakamilisha miezi saba.