Dikrii mbili za kushangaza za Aguila Saleh huko Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i9598-dikrii_mbili_za_kushangaza_za_aguila_saleh_huko_libya
Aguila Saleh Spika wa bunge la Libya amemteua mtawala wa kijeshi wa kieneo katika kipidi hiki cha kufanyika hamasisho la wote dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 20, 2016 03:29 UTC
  • Dikrii mbili za kushangaza za Aguila Saleh huko Libya

Aguila Saleh Spika wa bunge la Libya amemteua mtawala wa kijeshi wa kieneo katika kipidi hiki cha kufanyika hamasisho la wote dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh.

Libya ingali inakabiliwa na migopgoro mbalimbali ya kiusalama. Licha ya serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya kuanza shughuli zake, lakini serikali na bunge za zamani zingali zinaendelea na shughuli zao. Pamoja na hayo lakini inaonekana kuwa kuna muafaka wa kiwango fulani kuhusu shughuli za serikali hiyo ya umoja wa kitaifa.

Hii ni katika hali ambayo magaidi wa Daesh pia wamefanikiwa kupanua satwa yao huko Libya kwa kustafidi na hali ya ukosefu wa amani ndani ya nchi hiyo; kiasi kwamba kuna serikali ya Daesh inayoendesha shughuli zake katika Libya sasa mbali na ile ya umoja wa kitaifa na zile zilizokuwepo kabla ya hapo.

Hali hii inalifanya suala la mapambano dhidi ya magaidi wa Daesh katika maeneo mbalimbali ya Libya kuwa moja ya matukio yanayopewa kimbaumbele nchini humo. Jukumu la kuendesha vita dhidi ya magaidi wa Daesh limepatiwa jeshi la taifa la Libya chini ya uongozi wa kamanda Khalifa Haftar. Hata hivyo Khalifa Haftar anahesabiwa kuwa mmoja wa vyanzo vya hitilafu kati ya serikali ya umoja wa kitaifa na wapinzani wa serikali hiyo. Hii ni kwa sababu Fayez al Sirraj Waziri Mkuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya anasema kuwa Khalifa Haftari hana wadhifa mwingine ghairi ya kuwa kamanda wa jeshi, licha ya wapinzani wa Libya kusisitiza kuwa kamanda huyo anapaswa kushiriki katika vikao vya baraza la mawaziri.

Katika upande mwingine ni kuwa, Aguila Saleh Spika wa bunge la Libya ametangaza zoezi la kuhamasishwa watu kote nchini humo kwa lengo la kupambana na Daesh, na katika hatua yake ya kushangaza amemteuwa Meja Jenerali Abdallah al Nadhuri Mkuu wa majeshi ya Libya kuwa mtawala wa kijeshi wa eneo linaloanzia huko Derna mashariki mwa Libya hadi bin Jawad magharibi mwa nchi hiyo.

Aguila Saleh amechukua hatua hiyo ya kushangaza katika hali ambayo kabla ya hapo spika huyo aliwekewa vikwazo na Wizara ya Fedha ya Marekani kutokana na kile kilichotajwa na wizara hiyo kuwa kukwamisha kuhitimishwa utawala wa serikali mbili na kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa huko Libya. Aguila Saleh pia ametoa radiamali yake kwa uamuzi huo wa Washington na kuutaja kuwa usio na maana wala thamani yoyote. Amesema uamuzi huo hauna maana kwa sababu yeye hana fedha zozote nje ya Libya wala katika benki za eneo ambazo zinaweza kuzuiliwa. Hatua ya Aguila Saleh ya kumteuwa mtawala wa kijeshi wa kieneo huko Libya kutoka miongoni mwa wale waliokuwa wakiunga mkono kuendelezwa wadhifa wa Abdallah al Thani Waziri Mkuu wa serikali ya Tobruk, inatathmini kuwa ni sawa na kuyaangamiza makubaliano ya Sakhirat na kuendeleza utawala wa serikali mbili huko Libya.