Upatanishi wa Wazayuni Sudan; kisingizio kingine cha kujipenyeza
(last modified Wed, 26 Apr 2023 10:58:44 GMT )
Apr 26, 2023 10:58 UTC
  • Upatanishi wa Wazayuni Sudan; kisingizio kingine cha kujipenyeza

Katika hali ambayo mgogoro wa Sudan pamoja na vita vinaendelea kushuhudiwa, utawala haramu wa Israel umewaalika majerali mahasimu wa Sudan kwenda Tel Aviv kwa ajili ya upatanishi.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya utawala bandia wa Israel amesema kuhusiana na hili kwamba, Israel imependekeza iwe mwenyeji wa mazungumzo baina ya Abdul-Fattah al-Burhan kamanda wa jeshi la Sudan na Muhammad Hamdan Dagalo, mkuu wa kikosi cha radiamali ya haraka.

Katika miaka ya hivi karibuni, viongozi wa Sudan wamefanya hima ya kufuata siasa na matakwa ya Marekani ili kwa njia hiyo waweze kuimarisha nafasi ya Israel na wakati huo huo wanufaike na misaada ya Marekani na washirika wake. Katika uwanja huo, serikali ya Sudan ilikubali kuutambua rasmi utawala haramu wa Israel na kuanzisha nao uhusiano wa kawaida mkabala wa kupewa misaada na Marekani. Ni kwa utaratibu huo kukaanza mahusiano rasmi baina ya Sudan na utawala huo vamizi.

Bara la Afrika na hususan mataifa kama Sudan kutokana na kuwa na vyanzo vya utajiri na maliasili kama madini, kuwa katika eneo muhimu la kijiografia, kwa miongo kadhaa sasa nchi hiyo imekuwa ikizingatiwa na kukodolewa macho ya tamaa na utawala haramu wa Israel. Siku zote Israel imekuwa ikifanya juhudi kuhakikisha kwamba, inakuwa na ushawishi katika nchi hiyo ikitumia mazingira mbalimbali yanayojitokeza ili kwa njia hiyo iweze kufikia malengo yake. Mfano wa wazi ni kujitenga Sudan Kusini na Sudan ambapo katika kadhia hiyo kuna ishara za wazi na bayana za kuweko mkono wa Israel katika kadhi hiyo.

Ripoti ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa inaonyesha kuwa, wakati Sudan Kusini inapigania kujitenda na Sudan, utawala haramu wa Israel ulikuwa ukituma silaha Sudan Kusini na hivyo kuvifanya vita vya ndani kuchukua muda mrefu. Hatimaye vita hivyo vilipelekea kujitenga Sudan Kusini na Sudan.

Majerali hasimu kwa sasa nchinii Sudan

 

Isam Iwadh Mutawali balozi wa zamani wa Sudan nchini Algeria anasema: Utawala wa Kizayuni wa Israel ulikuwa na nafasi kuu na ya kimsingi katika kujitenga Sudan Kusini na kwamba, Israel ilikuwa na mpango wa kuhakikisha maeneo mengine ya Sudan pia kama Darfur yanajitenga lakini haikufanikiwa.

Katika miaka ya hivi karibuni Israel imeongeza juhudi zake kwa ajili ya kuwa na upenyaji na ushawishi zaidi barani Afrika na kwa kuzingatia migogoro ya kisiasa na kiuchumi ya Sudan iliandaa uwanja uwanja wa Sudan kuanzisha uhusiano wa kawaida na Tel Aviv.

Katika uwanja huo, mtandao wa habari wa Deutsche Welle umeandika katika moja ya makala zake kwamba: Sudan ina umuhimu mkubwa wa kistratejia kwa Tel Aviv. Israel ipo katika eneo ambalo linakaribiana na Misri, Sudan Kusini, Uganda na Eritrea na hivyo kwa kuifanya Sudan kuwa miongoni mwa washirika na waitifai wake itaweza kupanua wigo wa ushawishi wake barani Afrika.

Hata hivyo juhudi za Israel za kupenya na kuwa na ushawishi huko Sudan zimekabiliwa na malalamiko makubwa ya wananchi wa nchi hiyo.

Walid al-Iwadh, mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Sudan anasema: Ushirikiano wa jenerali Abdul-Fattah al-Burhan na Wazayuni utachora ramani ya senario yenye msiba na majanga kwa Wasudan na utapanua wigo wa chuki na hasama na wakati huo huo kuwa na taathira hasi kwa mchakato wa kuangalia upya ramani ya njia ya miungano ya kitaifa ndani ya Sudan.

Uingiliaji wa kigeni katika masuala ya ndani ya Sudan katika miezi ya hivi karibuni umeifanya hali ya Sudan kuwa mbaya zaidi. Hali imezidi kuwa mbaya hasa baada ya kuzuka mapigano baina ya jeshi la Sudan na kikosi cha radiamali ya haraka, vita ambavyo vitazidi kuifungulia mlango Israel. Weledi wengi wa mambo wanaamini kuwa, Israel ina mkono katika vita hivyo.

Wakimbizi wanaendelea kuongezeka nchini Sudan baada ya mapigano kushadidi nchini Sudan

 

Muhammad Jamal Arafa, mtaalamu na mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Sudan anasema:  Matukio ya Sudan yanajiri kwa namna ambayo endapo hali hiyo itaendelea nchi hiyo itakabidhiwa kwa wavamizi wa Kizayuni.

Anatahadharisha kwamba,  mapigano baina ya jeshi la Sudan linaloongozwa na Jenerali Abdul-Fattah al-Burhan na Muhammad Hamdan Dagalo, mkuu wa kikosi cha radamali ya haraka yanaweza kupelekea kuigawa Sudan na hivyo kutekelezwa mipango yya makundi yanayopigania kujitenga ambayo yanafanya harakati zao katika kuhudumia malengo ya utawala haramu wa Israel na Marekani.

Hatua ya kimaonyesho ya utawala haramu wa Israel ya kuwaita huko Tel Aviv majenerali hasimu katika kikao ambacho kidhahiri ni cha kutafuta upatanishi na upande mwingine wa sarafu wa juhudi za Wazayuni za kutaka kueneza satuwa na ushawishi wao katika nchi ya Kiislamu tena katika eneo muhimu la Pembe ya Afrika na Ukanda wa Mto Nile.

Tags