Maelfu ya familia za Wasudani zakimbilia Misri wakihepa mapigano
Maelfu ya wananchi wa Sudan wamevuka mpaka wa Arqin wa kaskazini mwa nchi hiyo na kuingia Misri wakikimbia mapigano yanayoendelea nchini kwao kati ya Jeshi la Taifa na vikosi vya jeshi la Radiamali ya Haraka (RSF) yaliyoanza katikati ya mwezi huu.
Habari zinasema kuwa, mabasi yameonekana yakiwa yamepanga foleni katika eneo la mpaka wa Sudan na Misri; ambapo wananchi wa Sudan wamelala nje katika maeneo ya jangwani, wakisubiri ruhusa ya kuingia katika nchi jirani ya Misri.
Nawal al Sharif, raia wa Sudan amenukuliwa akisema kuwa; ameyaacha makazi yake kwa sababu ya mapigano kati ya wenyewe kwa wenyewe.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imesema kuwa wakimbizi zaidi ya 14,000 kutoka Sudan wamevuka mpaka na kuingia nchini humo tangu kuanza mapigano makali huko Sudan.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imeongeza kuwa, hadi sasa raia 2,000 wa nchi nyingine 50 au wawakilishi wa taasisi za kimataifa pia wamevuka mpaka au wamesafirishwa kwa ndege hadi Misri kufuatia mapigano yanayoendelea huko Sudan.
Huku haya yakiripotiwa, Wizara ya Afya ya Sudan imetangaza kuwa watu wasiopungua 512 wakiwemo raia wa kawaida na wanajeshi wameuawa na wengine 4,200 kujeruhiwa tangu kuanza mapigano mwezi huu nchini humo.
Shirika la Madaktari linalofuatilia vifo vya raia, limetangaza kuwa takriban raia 295 wameuawa na wengine 1,790 wamejeruhiwa.