Mpango wa Chakula Duniani (WFP) waondoa zuio la oparesheni zake huko Sudan
(last modified Tue, 02 May 2023 01:31:20 GMT )
May 02, 2023 01:31 UTC
  • Mpango wa Chakula Duniani (WFP) waondoa zuio la oparesheni zake huko Sudan

Mpango wa Chakula Duniani (WFP) umetangaza kuwa umeamua kuondoa zuio la oparesheni zake za misaada ya kibinadamu nchini Sudan ambalo liliwekwa kufuatia kifo cha kusikitisha cha mfanyakazi mmoja wa shirika hilo hivi karibuni.

Cindy McCain Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la WFP amesema kuwa shirika hilo linaanza tena kutekeleza oparesheni zake za kibinadamu kwa kuzingatia mahitaji makubwa ya sasa ya raia wengi wa nchi hiyo.

Mpango wa Chakula Duniani tarehe 16 mwezi huu ulisema kuwa unasitisha kwa muda oparesheni zake zote za kibinadamu huko Sudan baada ya wafanyakazi wake wawili kuuliwa siku hiyo katika mapigano kati ya jeshi la Sudan na vikosi vya radiamali ya haraka (RSF). 

Wakati huo huo Abdallah Hamdok Waziri Mkuu wa zamani wa Sudan ametahadharisha kuwa mapigano yanayoendelea nchini humo yanaweza kushtadi na kuwa moja ya vita vibaya zaidi vya wenyewe kwa wenyewe kuliko vile vilivyoshuhudiwa huko Syria na Libya kama pande hasimu hazitasimamisha mapigano.  

Waziri wa zamani wa Sudan,Abdallah Hamdok 

Hamdok amewatolea wito majenerali wanaopigana kusimamisha vita na kufikia mapatano.

Tags