Mlipuko mkubwa waripotiwa katikati ya mji mkuu wa Sudan, Khartoum
Ripoti zinasema kuwa sauti ya mlipuko mkubwa imesika katikati ya mji mkuu wa Sudan, Khartoum leo asubuhi.
Mapigano na ghasia kubwa zilianza katika maeneo mbalimbali na hasa katika mji mkuu wa Sudan Khartoum kati ya vikosi vya jeshi la Sudan vinavyoongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Burhan na wanamgambo wa kikosi cha radiamali ya haraka (RSF) kinachoongozwa na Muhammed Hamdan Dagalo maarufu kwa jina la Hamidati tangu Aprili 15 mwaka huu.
Mapigano hayo hadi sasa yameuwa watu wasiopungua 600.
Televisheni ya al Jazeera imetangaza mapema leo kwamba mlipuko mkubwa umetokea katikati mwa Khartoum;ambapo moshi umeonekana ukisambaa hewani katika maeneo ya pambizoni mwa ikulu ya Rais.
Televisheni ya al Jazeera imeongeza kuwa ndege za kivita za jeshi la Sudan linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Burhan zimeonekana zikiruka katika anga ya mji mkuu Khartoum na katika mji wa Khartoum Kaskazini ambapo zilikuwa zikiushambulia upande wa mahasimu wao yaani wanamgambo wa kikosi cha radiamali ya haraka chini ya uongozi wa Muhammed HamdanDagalo.
wakati huo huo sauti za milipuko miwili zimesikia pia katika mji wa Khartoum ya Kaskazini. Mapigano na milipuko yote hii inaripotiwa kushuhudiwa huko Khartom katika hali ambayo Jenerali al Burhan na hasimu wake Hamidati tayari wamekubaliana kusitisha vita kwa muda wa wiki moja kuanzia kesho Alhamisi.