Boko Haram washambulia mazishi Cameroon; waua 6 na kujeruhi 30
Watu wasiopungua sita wameuawa na wengine 30 wamejeruhiwa wakati magaidi wawili wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram walipojiripua kwenye umati wa watu waliokuwa kwenye shughuli ya mazishi ya Waislamu katika eneo la Nguetchewe nchini Cameroon.
Maafisa wa serikali ya Cameroon katika eneo hilo lililoko umbali wa kilomita 10 mashariki mwa mpaka wa nchi hiyo na Nigeria wamesema shambulio hilo la leo ni la kwanza kufanywa na Boko Haram kulenga mkusanyiko wa mazishi ya Waislamu, japokuwa huko nyuma waliwahi kushambulia hafla ya ubatizo ya wafuasi wa Kikristo.
Kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram ambalo ngome yake kuu ni kaskazini mashariki mwa Nigeria limeshadidisha mashambulio yake nje ya mipaka ya nchi hiyo hadi ndani ya eneo la kaskazini mwa ardhi ya Cameroon licha ya kuundwa kikosi imara cha askari wapatao 9,500 kutoka nchi za kanda ya magharibi mwa Afrika cha kupambana na kundi hilo.
Mbali na Cameroon, mashambulio ya magaidi wa kundi la kitakfiri la Boko Haram yamekuwa yakizilenga nchi za Chad na Niger ambazo pia zinapakana na Nigeria. Inadaiwa kuwa kuna wanamgambo 8,700 wa Boko Haram kwenye eneo hilo la magharibi mwa bara Afrika.
Tangu lilipoanzisha uasi mwaka 2009, kundi hilo la kigaidi na kitakfiri limehusika na mashambulio chungu nzima ya utumiaji silaha na utegaji mabomu katika maeneo mbalimbali ya Nigeria ambayo yamesababisha watu wapatao 13,000 kuuawa na wengine zaidi ya milioni moja na nusu kulazimika kuyahama makazi yao ikiwa ni pamoja kukimbilia nchi jirani ikiwemo Chad na Cameroon.../