Juhudi za kuleta mapatano nchini Sudan
Katika hali ambayo vita nchini Sudan vimeingia katika wiki yake ya tatu juhudi za kieneo na kimataifa za kusitisha vita na kuzishajiisha pande mbili kukaa katika meza moja ya mazungumzo ili kuupatia ufumbuzi mzozo huo zinaendelea.
Matunda ya karibu kabisa ya juhudi hizo ni kufikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano kwa muda wa wiki moja yaliyoanza kutekelezwa hapo jana Alkhamisi. Ripoti zinasema, kiongozi wa jeshi la Sudan Abdul-Fattah al-Burhan na mkuu wa kikosi maalumu cha usaidizi wa haraka, RSF, Mohammed Hamdan Daglo, wamekubaliana juu ya mkataba wa usitishwaji mapigano kwa siku saba kuanzia jana Alkhamisi Mei 4 hadi Alkhamisi wiki ijayo Mei 11. Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Sudan Kusini. Taarifa hiyo imetolewa siku chache baada ya Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir kuanza mazungumzo ya upatanishi kati ya pande hizo mbili zinazohasimiana, kama mwakilishi wa shirika la maendeleo la nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na pembe ya Afrika, IGAD.
Mapigano ya silaha nchini Sudan yalianza Aprili 15 kati ya vikosi vya jeshi la nchi hiyo chini ya uongozi wa Jenerali Abdul Fattah al-Barhan ambaye ni mkuu wa baraza la uongozi la Sudan na Mohammed Hamdan Dagalo maarufu kwa jina la "Hamidati" kamanda wa vikosi vya radiamali ya haraka (RSF).
Majerali hao wawili wa kijeshi ambao mwaka 2019 walikuwa kitu kimoja katika harakati za kuondolewa madarakani Rais Omar al-Bashir sasa wamekuwa mahasimu wakuu ambao wameitumbukiza Sudan katika vita na machafuko. Aidha walikuwa waitifaki mwaka 2021 katika mapinduzi ya kuhitimisha utawala wa kiraia. Wajuzi wa mambo wanaamini kwamba, hitilafu zilizoibuka baina ya wawili hao na kushindwa kuafikiana kuhusiana na kuunganishwa na jeshi Kikosi cha Usaidizi wa Haraka ndio chanzo kikuu cha pande mbili kuelekezeana mtutu wa bunduki.
Filihali mapigano nchini Sudan yamegeuka na kuwa vita kamili na mpaka sasa juhudi za kieneo na kimataifa za kuhitimishwa vita na kuzikinaisha pande mbili zikae katika meza moja ya mazungumzo bado hazijazaa matunda. Hata makubaliano kadhaa yaliyofikiwa kuhusiana na usitishaji vita nayo hayajaheshimiwa na pande mbili jambo linalodhihirisha ni kwa kiasi gani uhasama na uadui baina ya pande mbili umeshadidi.
Kila upande miongoni mwa pande mbili hasimu zinautuhumu upande mwingine kwamba, ndio unaobeba dhima na masuuliya ya hali ya sasa ya Sudan. Mapigano ya sasa ya Sudan yameuwa watu takribani 600.
Hospitali nyingi zimelengwa kwa mabomu, vifaa vya kibinadamu kuporwa na mashirika ya misaada ya kigeni kulazimika kusimamisha shughuli zao nyingi. Makumi ya maelfu ya Wasudan wamekimbilia nchi jirani katika misafara ambayo imepelekea kuwepo tahadhari kuhusu "janga" la kibinadamu na athari kwa eneo zima.
Takwimu mbalimbali za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa, karibu watu 400,000 wamelazimika kuwa wakimbizi tangu mapigano hayo yaanze katikati ya mwezi uliopita wa Aprili.
Kwa upande wake Shirika la Afya Duniani (WHO) linaonya kuwa wengi watakufa kutokana na ukosefu wa huduma muhimu na milipuko ya magonjwa. Aidha dawa zimepungua sana katika maeneo yaliyoharibiwa na mapigano, ikiwa ni pamoja na katika mji mkuu Khartoum pamoja na Darfur Magharibi na Kati.
Shirika la Mpango wa Chakula WFP linasema, vita hivyo sio mgogoro wa Sudan tu, bali endapo vitaendelea utageuka na kuwa mgogoro wa eneo zima.
Filihali kufuatia juhudi zilizofanyika, pande mbili zimekubali kusitisha vita kwa muda wa siku saba na imeafikiwa kuwa kuanze mazungumzo kwa shabaha ya kufikia makubaliano. Pamoja na hayo inaonekana kuwa, bado kuna kibarua kigumu mno mpaka kufikiwa lengo hilo.