UN: Idadi kubwa ya kutisha ya watoto wanaouliwa vitani Sudan
(last modified Sun, 07 May 2023 07:05:30 GMT )
May 07, 2023 07:05 UTC
  • UN: Idadi kubwa ya kutisha ya watoto wanaouliwa vitani Sudan

Umoja wa Mataifa wiki hii umetahadharisha kuwa idadi kubwa ya watoto wanakufa vitani huko Sudan, na kueleza kuwa ripoti zinaonyesha kuwa watoto saba walikuwa wakiuawa au kujeruhiwa kila saa nchini humo.

James Elder msemaji wa Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF ameeleza kuwa: Kama inavyohofiwa na kutahadharishwa, hali nchini Sudan imekuwa mbaya kufuatia idadi kubwa ya watoto kupoteza maisha. Ameongeza kuwa, Unicef imepokea taarifa kutoka mshirika mwaminifu hata hivyo ambazo hazijathibitishwa na Umoja wa Mataifa zikibainisha kuwa, watoto 190 waliuliwa na wengine 1,700 kujeruhiwa katika kipindi cha siku 11 za mapigano yaliyoanza Sudan Aprili 15 mwaka huu.  

Mapigano Sudan

Msemaji wa UNICEF ameeleza kuwa, takwimu zote hizi zimekusanywa kutoka vituo vya afya huko Khartoum na katika jimbo la Darfur. Amesema takwimu hizo zinahusiana na wale watoto waliofika kwenye vituo vya afya katika maeneo hayo tajwa. Mamiai ya watu wameuawa na mamia ya maelfu ya wengine wamelazimika kukimbia makazi yao huko Sudan tangu kuanza mapigano wiki tatu zilizopita kati ya vikosi vya jeshi la nchi hiyo na vikosi vya usaidizi wa haraka (RSF). 

Pande zinazozozana Sudan hadi sasa zimeshafikia mapatano ya kusitisha vita kwa mara kadhaa hata hivyo hakuna hata moja lililoheshimiwa kikamilifu, ambapo juzi Ijumaa mashambulizi ya anga na ufyatuaji risasi uliendelea kushuhudiwa katika mji mkuu wa Sudan Khartoum kwa siku 21 mtawalia. Wakati huo huo Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limebainisha wasiwasi wake kuhusu hali mbaya ya mambo huko Sudan na kuzitolea wito nchi mbalimbali kujiepusha na kuwarudisha raia wa Sudan nchini humo.

Tags