Mlipuko mkubwa waukumba mji mkuu wa Sudan, Khartoum mapema Jumatano
Mlipuko mkubwa umeukumba mji mkuu wa Sudan, Khartoum mapema leo katika siku ya 26 ya vita vya kuwania madaraka kati ya jeshi la nchi hiyo linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Burhan na vikosi vya Usaidizi wa Haraka (RSF) vinavyoongozwa na Kamanda Hamdan Dagalo.
Mkazi mmoja wa mji wa Omdurman, nje kidogo ya mji mkuu, Khartoum ameliambaia shirika la habari la AFP kwamba wameamshwa na milipuko na sauti kubwa za makombora. Usiku wa kuamkia leo pia mashuhuda katika vitongoji tofauti mjini Khartoum wamesema walisikia milipuko miwili mikubwa katika mji huo mkuu wenye jamii ya watu milioni tano. Wakazi wa mji wa El-Obeid umbali wa kilomita 350 Magharibi mwa Khartoum pia wamesema kuwa leo kulijiri mapigano na milipuko kadhaa katika mji huo.
Jenerali Abdel Fattah al Burhan mkuu wa baraza la uongozi wa kijeshi la Sudan na hasimu wake, Jenerali Mohamed Hamdane Dagalo anayeongoza vikosi vya RSF Jumamosi iliyopita walituma wasuluhishi wao nchini Saudi Arabia kwa ajili ya majadiliano ya awali ya kiufundi kuhusu masuala ya misaada ya kibinadamu.
Martin Griffiths Mkuu wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa ambaye aliwasili Jeddah siku ya Jumapili alipendekeza kuwa, pande mbili hasimu huko Sudan zinapasa kudhamini suala la ufikishwaji misaada ya kibinadamu kupitia tamko la hati ya kisheria.
Mapigano Sudan yameuwa watu zaidi ya 750 na wengine 5000 kujeruhiwa tangu yalipoanza tarehe 15 mwezi Aprili.
Karibu wakimbizi 150,000 wamekimbilia katika nchi jirani. Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa . Wakati huo huo idadi ya wakimbizi wa ndani nchini Sudan imepindukia laki saba; kiwango ambacho ni mara mbili ya kile kilichoripotiwa wiki iliyopita.