UN: Wakimbizi wa Sudan wanakabiliwa na maafa ya binadamu katika nchi jirani
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa wakimbizi wa Sudan wanakabiliwa na maafa ya binadamu katika nchi jirani.
Mapigano ya silaha nchini Sudan yalianza asubuhi ya Jumamosi, Aprili 15 mwaka huu kati ya vikosi vya jeshi la taifa na vikosi vya usaidizi wa haraka (RSF) huku jitihada za upatanishi wa kimataifa ili kuupatia ufumbuzi mgogoro wa pande hasimu zikiwa bado hazijazaa matunda.
Umoja wa Mataifa umesisitiza kuwa, tangu kuanza vita huko Sudan mwezi mmoja uliopita karibu raia laki mbili wa nchi hiyo wamekimbilia katika nchi jirani na wanakabiliwa na maafa makubwa.
Hadi sasa watu wasiopungua 750 wameuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa katika mapigano hayo.
Kwa kuzingatia hali ya usalama ya Sudan aghalabu ya majeruhi wa mapigano wameshindwa kufika hospitali kwa ajili ya matibabu na kwa sababu hii, inaonekana kwamba idadi ya waathirika na waliojeruhiwa inaweza kuwa kubwa zaidi kuliko takwimu za sasa.