May 26, 2023 10:08 UTC
  • Watoto 30 wameaga dunia hospitalini kutokana na mgogoro wa Sudan

Makumi ya watoto wachanga wa kuzaliwa wameaga dunia wakiwa hospitalini tangu vita vipya viibuke nchini Sudan mwezi uliopita, huku mapigano hayo yakiendelea kwa wiki ya sita sasa licha ya makubaliano ya usitishaji vita.

Hayo yamesemwa na Stephane Dujarric, Msemaji wa Umoja wa Mataifa ambaye ameeleza kuwa, watoto sita wameaga dunia wakiwa hospitalini ndani ya wiki moja katika mji wa Ed Daein, muda mfupi baada ya kuzaliwa kutokana na changamoto mbalimbali kama vile ukosefu wa hewa ya oksijeni na umeme.

Dujarric amenukuu takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinazoonesha kuwa, watoto zaidi ya 30 wamepoteza maisha wakiwa hospitaini tangu mgogoro huo uibuke nchini Sudan.

Mapigano hayo ya silaha yalianza tangu Aprili 15 mwaka huu kati ya vikosi vya jeshi na vikosi vya usaidizi wa haraka kuhusu uongozi wa nchi.

Msemaji wa UN amesema WHO inawasiliana na maafisa wa afya katika eneo hilo ili kujaribu kuupatia ufumbuzi mgogoro huo wa kibinadamu.

Mapigano Sudan

Mapigano hayo kati ya jeshi la Sudan na askari wa Kikosi cha Usaidizi wa Haraka (RSF) yameitumbukiza nchi hiyo kwenye lindi la machafuko.

Raia 863 wameripotiwa kuuawa kwenye mapigano hayo huku maelfu ya wengine wakijeruhiwa, mbali na zaidi ya watu milioni moja wakilazimika kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi.

Hifadhi ya chakula, fedha taslimu na vitu muhimu vinapungua kwa kasi, huku uporaji mkubwa ukiathiri benki, balozi, na maghala ya bidhaa za misaada nchini humo.

Tags