Jeshi la Sudan limesema limesitisha mazungumzo na vikosi pinzani
Msemaji wa jeshi la Sudan jana alieleza kuwa jeshi hilo limesitisha kushiriki katika mazungumzo na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) ambavyo limekuwa likipigana navyo kwa wiki kadhaa sasa kwa ajili ya kuidhibiti Sudan.
Weledi wa mambo wameutaja uamuzi huo wa jeshi la Sudan kuwa ni pigo kwa Marekani na Saudi Arabia ambazo zimekuwa zikijaribu kuzipatanisha pande mbili zinazopigana nchini Sudan.
Msemaji wa Jeshi la Sudan, Brigedia Nabil Abdalla, ameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba, wamefikia uamuzi huo ikiwa ni ishara ya kulalamikia kile alichokitaja kuwa ukiukaji wa mara kwa mara wa mapatano ya kusimamisha mapigano unaofanywa na vikosi vya RSF; ikiwa ni pamoja na kitendo cha vikosi hivyo pinzani cha kuendelea kuzidhibiti hospitali, baadhi ya majengo na miundombinu mingine ya raia katika mji mkuu Khartoum.
Sudan ilitumbukia katika hali ya mchafukoge baada ya kuzuka mapigano katikati ya mwezi Aprili mwaka huu kati ya jeshi la nchi hiyo linaloongozwa na jenerali Abdel- Fattah al Burhan na Kamanda wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo.
Hadi sasa mapigano hayo yameuwa raia wasiopungua 866 na kujeruhi maelfu ya wengine.
Brigedia Nabil Abdalla ameongeza kuwa, jeshi la Sudan linataka kuhakikisha kuwa masharti ya mapatano yanatekelezwa kikamilifu kabla ya kujadili hatua nyingine zaidi.
Jeshi la Sudan (SAF) na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) juzi walikubaliana kuongeza muda wa siku tano wa kusitisha mapigano. Makubaliano hayo yalitiwa saini na pande mbili tarehe 20 mwezi huu wa Mei 20 baada ya mazungumzo yaliyofanyika mjini Jeddah, Saudi Arabia.