Eswatini yaikosoa US kwa kuingilia masuala yake ya ndani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i98328-eswatini_yaikosoa_us_kwa_kuingilia_masuala_yake_ya_ndani
Serikali ya Eswatini imeukosoa vikali ubalozi wa Marekani kwa kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo ya kusini mwa Afrika.
(last modified 2025-10-17T12:36:14+00:00 )
Jun 03, 2023 01:32 UTC
  • Eswatini yaikosoa US kwa kuingilia masuala yake ya ndani

Serikali ya Eswatini imeukosoa vikali ubalozi wa Marekani kwa kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo ya kusini mwa Afrika.

Katika taarifa jana Ijumaa, Msemaji wa Serikali ya Eswatini, Alpheous Nxumalo amesema Utawala wa Kifalme wa Eswatini haujawahi kuingilia masuala ya andani ya nchi yoyote ile, na hivyo hauelewi ni kwa nini Washington inaingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo.

Nxumalo ameihutubu Marekani kwa kuhoji, "Swali la msingi ni je, ubalozi wa Marekani una haki gani ya kuingilia maamuzi ya mahakama ya Ufalme huu?"

Siku ya Alkhamisi, Mahakama Kuu ya Mbabane iliwahukumu wabunge wawili wa zamani wa Eswatini, Mduduzi Bacede Mabuza na Mthandeni Dube, karibu miaka miwili jela, kwa 'kuchochea ghasia zilizosababisha vifo.'

Muda mfupi baada ya kutolewa hukumu hiyo, ubalozi wa Marekani ulidai kuwa umeghadhabishwa na uamuzi huo wa makahama, na kuitaka serikali ya Eswatini kuwa na eti uwazi katika michakato ya kesi, kudumisha utawala wa sheria na kulinda haki binadamu.

Mfalme Mswati III wa Eswatini (Swaziland)

Akijibu bwabwaja hizo, Msemaji wa Serikali ya Eswatini, Alpheous Nxumalo amesema Marekani ilikiuka sheria za kimataifa kwa kuunda gereza la kutisha la Guantanamo Bay (Cuba), ili kuwazuilia eti washukiwa wa ugaidi.

Nxumalo amebainisha kuwa, licha ya watetezi wa haki za binadamu kulaani uamuzi huo na kutaka kufungwa gereza hilo, lakini Eswatini haikusema chochote.

Oktoba mwaka 2021, maandamano yalifanyika kila siku yakidai demokrasia huko Eswatini zamani ikiitwa Swaziland, ambapo waandamanaji walikuwa wakipaza sauti dhidi ya hali ya kiuchumi na kisiasa.