Kuendelea mgogoro huko Sudan na kufukuzwa Mjumbe wa UN nchini humo
(last modified Sun, 11 Jun 2023 12:28:58 GMT )
Jun 11, 2023 12:28 UTC
  • Kuendelea mgogoro huko Sudan na kufukuzwa Mjumbe wa UN nchini humo

Mgogoro wa kisiasa na vita vya kuwania madaraka vinaendelea kutokota nchini Sudan licha ya jitihada zote za kimataifa na kikanda zinazofanyika kwa ajili ya kurejesha amani nchini huko. Katika hatua ya karibuni, Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imemfukuza Volker Perthes aliyekuwa Mjumbe wa Umoja wa Mataifa na kumtaja kuwa mtu asiyetakikana nchini humo.

Kamanda Mkuu wa jeshi la Sudan, Abdel Fattah al Burhan,  amedai katika ujumbe uliotumwa Umoja wa Mataifa kwamba Perthes alimtaka Muhammad Hamdan Daghalo Kamanda wa vikosi vya Usaidizi wa Haraka (RSF) kuanzisha uasi. Al Burhan amesema, kuwepo wa Volker Perthes kama kiongozi wa ujumbe wa kidiplomasia wa UN nchini Sudan hakutasaidia utekelezaji wa majukumu ya ujumbe huo katika kipindi chaa mpito. 

Kamanda wa jeshi la Sudan  Abdel Fattah al Burhan 

Vita vinavyoendelea nchini Sudan vinatatiza juhudi za kusitisha mapigano na kufikisha misaada ya kibinadamu kwa raia wa nchi hiyo hadi. Kila upande katika mapigano hayo unaamini kuwa, unaweza kushinda vita hivyo; kwa msingi huo hakuna upande unaoafiki mapendekezo yaliyowasilishwa kwa ajili ya kusitisha mapigano.   

Mohamed Hamdan Dagalo anasisitiza kwamba, vikosi vyake vitaondoka katika uwanja wa vita baada ya kukomeshwa mapinduzi ya jeshi. Dagalo ameitaja hatua iliyochukuliwa na al Burhan kuwa ni mapinduzi na kumtuhumu kuwa ni msaliti na na kwamba anajaribu kuwarejesha madarakani viongozi wa serikali ya zamani wakiwemo wafuasi wa mtawala wa zamani wa Sudan, Omar al Bashir.  

Mtawala wa zamani wa Sudan, Omar al Bashir 

Katika mazingira hayo, nchi ajinabi pia zimezidisha uingiliaji wao katika masuala ya ndani ya Sudan, na kila moja inafanya kila iwezalo kwa kisingizio cha juhudi za kurejesha amani nchini humo, lengo likiwa ni kudhibiti utajiri na maliasili za Sudan. Kwa msingi huo, katika mgogoro huo baadhi ya nchi za kikanda zinamuunga mkono Jenerali al Burhan na nyingine zikiimhami na kumsaidia Dagalo.

Wakati huo huo Stephane Dujarric msemaji wa Umoja wa Mataifa amekanusha tuhuma zilizotolewa na Mkuu wa jeshi la Sudan, Abel Fattah al Burhan dhidi ya mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan. Akimnukuu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dujarric alisema: Kanuni ya kipengele cha kumtambua mtu kwamba hatakikani haitumiki kwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, na kutumia kanuni hiyo dhidi ya wajumbe wa taasisi hiyo ni kinyume na wajibu wa nchi kulingana na Mkataba wa Umoja wa Mataifa.

Ni wazi kuwa pande hasimu nchini Sudan kivitendo zimefunga njia ya usitishaji vita wa kuaminika na kuanza mazungumzo ya amani. Pamoja na hayo, mazungumzo yanaendelea ili kufikia mapatano baina ya pande mbili. Marekani na Saudi Arabia ambazo zimechukua nafasi ya upatanishia katika mzozo wa Sudan, zinasisitiza kuwa lengo la mapatano mapya ni kusaidia juhudi za kufikisha misaada ya kibinadamu kwa raia wa nchi hiyo, kuhitimisha machafuko na kusaidia hatua za kujenga hali ya kuamianiana kati ya pande mbili hasimu ili kuandaa mazingira ya kuanza tena mazungumzo mjini Jeddah. 

Mapigano yalipamba moto huko Sudan katika siku za karibuni ambapo baadhi ya balozi za nchi ajinabi, ukiwemo ubalozi wa Saudia, zilishambuliwa kwa mara nyingine tena. Katika upande mwingine, maafa ya binadamu huko Sudan yamezidisha haja na udharura wa kupelekwa misaada ya chakula, dawa na huduma za matibabu kwa majeruhi wa vita. 

Mpango wa Chakula Duniani (WFP) umetangaza kuwa mashambulizi yanayoendelea Sudan yanahatarisha  misaada ya kibinadamu iliyopangwa kugawiwa kwa karibu watu milioni nne na nusu. Vilevile kupororwa vyakula na misaada ya kibinadamu kumedhoofisha kikamilifu mchakato wa usambazaji misaada hiyo kwa raia walioathiriwa na mapigano. 

Vita na mapigano ya dnani Sudan yamewalazimisha watu zaidi ya milioni moja na laki mbili kuwa wakimbizi ndani  ya nchi hiyo huku wengine karibu ya laki nne wakikimbilia katika nchi jirani. Katika kipindi cha wiki saba zilizopita pia mji mkuu wa Sudan, Khartoum, ulipata hasara na maafa makubwa, na miundomsingi muhimu ya mji huo imeharibiwa. 

Vita Sudan na kukimbia raia katika nchi jirani

Inaonekana kuwa katika hali kama hayo, kuwepo hitilafu kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan kunatatiza zaidi hali ya mambo nchini humo. 

Tags