Rais Kais Saied: Tunisia haitakuwa mlinzi wa mipaka ya Ulaya
(last modified Mon, 12 Jun 2023 04:40:47 GMT )
Jun 12, 2023 04:40 UTC
  • Kais Saied
    Kais Saied

Rais Kais Saied wa Tunisia amesema nchi hiyo haitakubali kufanywa gadi ya mpaka ya nchi za Ulaya, wakati huu ambapo safari za wahamiaji haramu kwenda Ulaya kupitia Bahari ya Mediterania zimeongezeka.

Shirika la habari la Reuters limemnukuu Rais wa Tunisia akisema hayo, muda mfupi kabla ya kukutana na viongozi wa Ulaya walioelekea katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika jana Jumapili.

Viongozi wa Ulaya walioko safarini Tunisia ni pamoja na Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni, mwenzake wa Uholanzi, Mark Rutte na Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen.

Rais Kais Saied amesisitiza kuwa, "Suluhu ya kukabiliana na wahamiaji haramu haitapatikana kwa gharama za Tunisia, hatutafanywa kuwa walinzi wa nchi hizi (za Ulaya)."

Wadadisi wa mambo wanasema kauli ya Rais wa Tunisia inakusudia kuyashinikiza madola ya Ulaya yaipe misaada zaidi ya kifedha nchi hiyo ya Kiarabu ambayo kwa sasa inakabiliwa na mdororo wa uchumi na mfumko wa bei.

Viongozi hao wa Ulaya wameahidi kuipa Tunisia msaada wa kifedha wa dola bilioni moja za kupambana na uhamiaji haramu. Aidha wameahidi kuwa nchi za EU zitawekeza kwenye sekta ya nishati jadidika kwa lengo la kurejesha uthabiti nchini humo.

Safari hatarishi za wahajiri kwenda Ulaya

Tunisia ni mojawapo ya vituo maarufu vya usafiri kwa wahamiaji haramu wenye azma ya kwenda Ulaya kutokana na kuwa katikati ya eneo la Bahari ya Mediterania.

Idadi ya wahamiaji wasio na vibali wanaojaribu kufika Italia kupitia Tunisia imekuwa ikiongezeka, licha ya hatua kali zinazochukuliwa na serikalli ya Tunisia kukabiliana na wahamiaji hao. Mara kwa mara, Gadi ya Pwani ya Tunisia imekuwa ikizima majaribio ya wahamiaji haramu kwenda Ulaya hasa kupitia fukwe za Italia katika Bahari ya Mediterania.