Mahakama Tanzania yaitaka serikali kutekeleza marekebisho ya sheria ya ndoa
(last modified Fri, 23 Jun 2023 02:38:02 GMT )
Jun 23, 2023 02:38 UTC
  • Mahakama Tanzania yaitaka serikali kutekeleza marekebisho ya sheria ya ndoa

Mahakama Kuu ya Tanzania Masijala ya Dar es Salaam imeipa serikali ya nchi hiyo miezi sita ya kutekeleza maamuzi ya mahakama yanayohusu marekebisho ya sheria ya ndoa juu ya umri wa mtoto wa kike kuolewa.

Chini ya wakili wa kujitegemea John Seka, shirika la kutetea maslahi ya wanawake na watoto, WOCWELS, lilifungua kesi hiyo katika Mahakama kuu ya Tanzania masijala ya Dar es Salaam, likipinga mchakato wa serikali kupitia wizara ya katiba na sheria wa kukusanya maoni kuhusu umri wa mtoto wa kike kuolewa, huku katika dodoso la maoni hayo wizara ikiutaja umri wa mtoto wa kike kuolewa kuwa ni miaka 14.

Kesi hiyo ya shirika la WOCWELS iliyofunguliwa mwaka jana 2022, iliitaka Mahakama kusitisha mchakato huo na badala yake wizara ya katiba na sheria ipeleke muswada wa bungeni, wa marekebisho ya sheria ya ndoa Tanzania ya mwaka 1971. Mwaka 2016, Makama kuu ya Tanzania ilimpa ushindi mwanaharakati Rebeca Gyumi aliyekuwa akipinga baadhi ya vifungu katika sheria ya ndoa nchini Tanzania, inayohalalisha mtoto wa kike kuolewa akiwa na umri wa miaka 14.

Kwenye kesi ya mwanaharakati Rebeca Gyumi iliamriwa kwamba umri wa mtoto kuolewa uwe ni miaka 18 na serikali ikakata rufaa kwa sababu haikuridhika na uamuzi huo lakini hata hivyo ilishindwa na sheria ilitakiwa kubadilishwa.

Lakini katika hali isiyokuwa ya kawaida wizara ya sheria na katiba ilianza kukusanya maoni ya wadau kuhusu umri wa mtoto wa kike kuolewa, badala ya kupeleka muswada wa mabadiliko ya sheria hiyo bungeni. Mbali na kutolewa maamuzi hayo, lakini pia mahakama imekemea mwenendo wa serikali ya Tanzania kusita sita ama kutotekeleza baadhi ya maamuzi ya Mahakama za ndani na za kimataifa.