Jul 10, 2023 02:44 UTC

Naibu Mufti na ambye pia ni mjumbe wa Baraza Kuu la Waislamu la Uganda amelaani kuchomwa moto Qur'ani Tukufu huko Sweden na kuitaja hujuma hiyo kuwa ni kitendo cha kinyama cha uchochezi dhidi ya dini yenye wafuasi zaidi ya bilioni mbili.

Ripota wa Iran Press huko Kampala mji mkuu wa Uganda amezungumza na Naibu Mufti wa Uganda Sheikh Muhammad Ali Waiswa ambaye ameitaka Sweden kuimarisha hatua za kukabiliana na chuki za kidini na kuongeza kuwa, uhuru wa kujieleza usiwe ni haki isiyo na mipaka. Amesema haki hiyo haiwezi kutumiwa kwa namna ambayo inadhalilisha haki na utu wa wengine. 

Sheikh Muhammad Ali Waiswa ameongeza kuwa kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu huko Sweden si kitendo cha kwanza kuwahi kushuhudiwa dhidi ya kitabu hicho cha mbinguni na kumvunjia heshima Mtume Muhammad (s.a.w). Kwa sababu huko nyuma pia,  hujuma kama hii ilishuhudiwa pia huko Denmark ambapo Waislamu wote inapasa walaani vikali vitendo hivi. 

Naibu Mufti wa Uganda amesisitiza kuwa, ulimwengu wa leo unatilia mkazo juu ya mawasiliano na kushirikiana baina ya dini mbalimbali, na katika mazingira hayo kuitusi Qur'ani Tukufu ni kitendo kisichokubalika na cha kinyama. 

Mjumbe huyo wa Baraza Kuu la Waislamu la Uganda pia amesema: Qur'ani Tukufu ni muujiza mkubwa wa Uislamu; na huu ni uhakika kwa sababu Qur'ani Tukufu inasomwa na kuhifadhiwa na mamia ya mamilioni ya watu duniani.  

Sheikh  Muhammad Ali Waiswa amebainisha kuwa wale wanaoiamini Qur'ani Tukufu kama kitabu cha Mwenyezi Mungu wanafahamu kuwa ni jambo la dharura kukiheshimu kitabu hicho cha mbinguni kwa sababu dhamira na ujumbe mkuu wa Uislamu ni kuleta amani. 

Jioni ya Jumatano  ya tarehe 28 Juni, Msweden mwenye asili ya Iraq anayejulikana kwa jina la "Salwan Momika" (umri wa miaka 37) alirarua nakala ya Qur'ani na kuichoma moto mbele ya Msikiti Mkuu wa Stockholm katika siku ya kwanza ya sikukuu ya Idul Adh'haa. Kitendo hicho kiovu kilifanyika chini ya ulinzi na himaya ya polisi ya Sweden.

Salwan Momika

 

 

 

Tags