Iran na Oman zafanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi + Video
(last modified 2024-10-11T02:38:53+00:00 )
Oct 11, 2024 02:38 UTC
  • Iran na Oman zafanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi + Video

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na jirani yake Oman zimefanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi yaliyoshirikisha Jeshi la Majini la Iran, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran SEPAH na Jeshi la Majini la Oman.

Taarifa rasmi inasema kuwa mwenyeji wa luteka hiyo ya pamoja ya kijeshi ilikuwa Oman na imefanyika kaskazini mwa Bahari ya Hindi ya Lango Bahari la Hormoz.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mazoezi hayo yamefanyika kwa mujibu wa makubaliano ya siku nyingi ya nchi hizi mbili ndugu, kwa ajili ya kuyaweka imara zaidi majeshi hayo ya ulinzi na ya kujihami, sambamba na kulinda kwa pamoja usalama wa maeneo hayo muhimu sana.

Manuwari kubwa ya kijeshi ya Jamaran iliyotengenezwa kikamilifu na wataalamu wa Iran pamoja na meli nyingine za kivita za Jamhuri ya Kiislamu zimeshirikiana na vyombo vingine vya kijeshi vya Oman katika mazoezi hayo.

Akizungumzia luteka hiyo, Kamanda wa Vikosi vya Ardhini vya Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Kioumars Heydari amesema kuwa, Jeshi la Oman ndilo lililopendekeza kufanyika mazoezi hayo ili kujiimarisha zaidi katika vita dhidi ya ugaidi. Hii ni mara ya kwanza kwa vikosi vya aina hizo tatu kufanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi.

Iran na Oman ni nchi mbili jirani zenye uhusiano mzuri katika kona mbalimbali. Wananchi wa mataifa haya mawili wana utamaduni unaofananaa na kwa miaka mingi nchi hizi zimefanya juhudi kubwa za kutunza ujirani mwema bila ya kuathiriwa na matukio mbalimbali mazito yanayotokea kwenye ukanda wa Asia Magharibi. 

Tags