Kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina; Jinai mpya dhidi ya Wapalestina
(last modified Thu, 20 Feb 2025 08:10:07 GMT )
Feb 20, 2025 08:10 UTC
  • Kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina; Jinai mpya dhidi ya Wapalestina

Leo tutaangazia jinai mpya ya Wazayuni na washirika wao ya kutaka kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina katika makazi na nchi yao.....

Hapa ni Gaza... Ni ukanda mwembamba unaozingirwa kutokea pande zote kwa miaka mingi na umeathiriwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya Wazayuni, lakini bado unaendelea kusimama imara na ngangari. 

Gaza ni makazi ya watu ambao wanaishi katika mashambulizi mtawalia ya utawala haramu wa Israel, na nchi ya watoto ambao badala ya kulala usingizi kwa kusikiliza hadithi na visa vya mama na bibi zao, wanalala wakisindikiswa na sauti za risasi, mizinga na milipuko ya mabomu, au vilio na mayowe ya majirani zao ambao wanaomboleza vifo vya wapendwa wao. Sasa watu hao wanaoishi kwenye dimbwi la masaibu kwa miaka mingi, wanawajihiana na jinai mpya! Jinai ya kuhamishwa kwa lazima kutoka kwenye nchi na makazi yao. 

Pendekezo jipya ambalo watenda jinai wameliweka mezani ni miongoni mwa mambo yanayovunja na kukiuka haki za msingi za binadamu katika mfumo wa sasa wa kimataifa,  kwa mujibu wa Azimio la Haki za Kibinadamu, Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia, Mkataba wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) na makumi ya hati nyinginezo za kisheria. Kwa miaka mingi Gaza imeathiriwa na mawimbi ya mashambulizi ya kikatili ya utawala bandia wa Israel, na ukanda huo mwembamba kwa miaka mingi sasa unahesabiwa kuwa moja ya maeneo yenye migogoro mikubwa duniani kutokana na uhalifu wa utawala wa Kizayuni. Hali hii imepelekea kukaririwa ukiukaji wa haki za binadamu ikiwa ni pamoja na kuwahamisha kwa nguvu mamilioni ya wakazi wa Gaza ndani na nje ya eneo hilo. 

Katika matamshi yake ya kipuuzi, hivi karibuni Rais wa Marekani, Donald Trump, aliitaja Gaza kuwa ni sehemu iliyoharibiwa na kwamba eti ni vyema wakazi wake  wakahamishwa na kupelekwa katika nchi nyingine. Trump amezungumzia suala la kuharibiwa eneo la Gaza, lakini hakutaja msababishaji wa maafa na uharibifu huo, yaani utawala wa Kizayuni wa Israel ambao ni rafiki na wmana mdekezwa wa muda mrefu wa Marekani. Rais wa Marekani ametangaza wazi kuwa nchi kama Misri, Jordan na kadhalika zinapaswa kuwapokea wakazi wa Gaza ili aweze kutekeleza mpango wake katika eneo hilo wa kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina, kutekeleza mauaji ya kisasa ya kimbari na kuendeleza sera za kibaguzi za utawala wa Kizayuni. Trump amependekeza kwamba wakazi wa Gaza wanapaswa kuondoka katika ardhi yao! Lakini je, waelekee wapi? waende msituni? au katika nchi za Kiarabu ambazo  siku zote zitawatambua raia hao kama wakimbizi? 

Hakuna shaka kuwa mpango na pendekezo la Donald Trump ni aina fulani ya kusasisha jinai kongwe ambazo Israel imekuwa ikizitekeleza tangu utawala huo bandia ulipoundwa. Jinai kama vile mauaji ya halaiki ya Deir Yassin na Sabra na Shatila hadi ujenzi wa ukuta wa kibaguzi unaotenganisha Gaza na meneo mengine yaliyoghusubiwa ya Palestina na kuzingirwa eneo hilo. Hivi sasa badala ya mashambulizi, Trump anataka kuwatenganisha wakazi wa Gaza na nchi yao, lengo likiwa ni kufuta utambulisho wa Palestina. Trump si mwanasiasa wa kwanza kuwahi kutoa pendekezo kama hili na bila shaka hatakuwa wa mwisho. Mpango huu ni mwendelezo wa sera ile ile iliyoanza mwaka 1948; yaani kuvamia ardhi ya Palestina, kuwahamishwa wakazi wake kwa mabavu na kubadilisha muundo wa idadi ya watu wa Palestina. 

Sasa tunakuja katika swali hili kwamba: Kwa nini wazo hili limeibuliwa tena? Jibu la swali hili jepesi sana, na kwa mujibu wa hali ya sasa tunaweza kusema kuwa, baada ya vita vya Gaza na kuongezeka uungaji mkono wa kimataifa kwa mapambano ya ukombozi ya Wapalestina, Israel ambayo imeshindwa kufikia malengo yake katika vita na mauaji ya kimbari ya miezi 15 dhidi ya wakazi wa Gaza licha ya kuharibu asilimia 85 ya miundo mbinu ya ukanda huo, sasa inataka kuwahamishwa kwa nguvu Wapalestina kwa mtindo mwingine, yaani kuwahamisha kwa nguvu.

Ni wazi kuwa, kwa kutoa pendekezo hilo, Trump anataka kuendeleza mpango wake wa "Muamala wa Karne" au kwa jina jingine Mpango wa Mashariki ya Kati Mpya ambao uligonga mwamba katika muhula wa wake wa kwanza wa urais. Hivi sasa na kwa kuzingatia hali ya Gaza; kidhahiri inaonekana kuwa Trump anataka anataka eneo hilo lijengwe upya lakini baada ya ujenzi huo, ardhi hiyo haitakuwa tena nchi ya Wapalestina, na kwa utaratibu huo Israel itakuwa imefikia lengo lake ovu inalolifuatilia kwa miaka mingi, yaani kufuta kizazi cha Wapalestina.  

Hata hivyo inatupasa kusema kuwa, mpango huu utaendelea kuwapo kwenye karatasi na ndoto za Trump tu, na si kwa mujibu wa uhakika wa mambo na historia, kwa sababu ardhi ya Gaza ni makazi ya asili ya enzi na enzi ya Wapalestina, ambao abadan hawatatoka katika makazi yao. 

Jibu la wananchi wa Palestina kwa mpango uliopendekezwa na Donald Trump liko wazi kikamilifu. "Ardhi hii ni nyumbani kwetu na hatutayahama makazi yetu."   

Wasikilizaji wapenzi tunawashukuru kwa kuendelea kutegea sikio makala yetu hii. Sasa hebu tutupie jicho mitazamo wa weledi wa masuala ya kimataifa na wanasiasa kwa njama hii ya Trump ya kutaka kuwahamishwa kwa nguvu Wapalestina. 

Olivier Corten, mhadhiri wa sheria za kimataifa katika Chuo Kikuu cha Brussels anasema kuhusiana na suala hili kwamba: "Iwapo mamia ya maelfu ya Wapalestina watahamishwa kwa nguvu kutoka katika ardhi yao, hatua hiyo  itakuwa na maana ya kupelekwa uhamishoni."

Corten anaamini kuwa hatua ya kutwaa na kudhibiti ardhi ya nchi nyingine bila kufikia mapatano au maelewano na nchi hiyo ina maana ya kuikalia kwa mabavu nchi hiyo; na iwapo nguvu  itatumika katika mchakato huo, hatua hiyo inakuwa ni "uchokozi". 

Wakati huo huo, wataalamu wa Umoja wa Mataifa wametangaza katika taarifa yao kwa vyombo vya habari kwamba ukiukaji huo wa wazi wa sheria unaofanywa na Marekani unavunja mwiko wa kanunii za kimataifa kuhusu uvamizi wa kijeshi na kuzipa ujasiri nchi nyingine kuvamia na kuyakalia kwa mabavu maeneo mbalimbali duniani na kusababisha athari hasi kwa amani ya kimataifa na haki za binadamu. Msemaji wa Umoja wa Mataifa pia amesema katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu mpango wa Trump wa kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina wa Gaza kwamba, umoja huo unapinga mpango huo na kwamba UN inapinga mpango wowote wenye lengo la kuwahamisha Wapalestina kutoka Ukanda wa Gaza au mpango wowote utakaopelekea kufutwa watu wa taifa moja. 

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas pia imetoa taarifa na kupinga mpango huo wa Trump. Hamas imesema kuwa inaendelea kusisitiza haki ya Wapalestina ya kubaki katika ardhi yao ya asili na inapinga hatua yoyote ya kuwahamisha kwa nguvu na kuwapeleka uhamishoni. 

Nchi na wanasiasa mbalimbali duniani pia wametangaza uungaji mkono wao kwa Palestina na kupinga mpango wa Donald Trump wa kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina.  

Jamii ya kimataifa sasa inapasa kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na Marekani ambayo ni mtetezi mkuu wa Israel ambayo inataka kuibua jinai nyingine mpya dhidi ya watu wa Palestina. Wakati umefika wa kutoka usingizini na kuvunja kimya cha miaka mingi kuhusu jinai za Israel na Marekani dhidi ya wananchi wanaodhulumika wa Ukanda wa Gaza. Nchi hizo zinapasa kusimama na kupinga vikali mpango wa Donald Trump ambao ni jinai kubwa dhidi ya binadamu.