Ulimwengu wa Spoti, Juni 9
(last modified Mon, 09 Jun 2025 06:18:08 GMT )
Jun 09, 2025 06:18 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Juni 9

Hujambo mskilizaji mpenzi, natumai u mzima wa afya hapo ulipo. Karibu tuangazie baadhi ya matukio muhimu yayojiri viwanjani ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa, kieneo na kimataifa…..

Voliboli: Iran mabingwa

Timu ya voliboli ya Iran 'B' imetwaa ubingwa wa Ligi ya Mataifa ya Wanaume ya Asia ya Kati CAVA ya mwaka huu 2025. Katika fainali ya aina yake iliyopigwa Jumatano, Iran iliitandika India seti 3-0 (25-17, 25-20, 25-19) na kuibuka kidedea. Iran ilitinga fainali baada ya kuzisasambua India 3-1, Turkmenistan 3-1, Uzbekistan 3-0, Kazakhstan 3-0, na Pakistan 3-1 katika mechi zao za awali huko Fergana nchini Uzbekistan. Pakistan ilipata medali ya shaba kwa ushindi mnono wa seti 3-1 dhidi ya Kazakhstan katika mchuano wa kutafuta mshindi wa tatu. Awali, michuano hiyo ya kibara ilipangwa kufanyika nchini Pakistan, lakini ilibidi ihamishiwe nchini Uzbekistan kutokana na mzozo uliokuwa umeshtadi baina yaPakistan na India.

Riadha: Muirani aweka historia Korea Kusini

Mwanamichzo wa Iran, Mahdi Olfati ameshinda medali ya dhahabu katika Mashindano ya Mazoezi ya Viungo ya Wanaume ya Asia ya 2025 nchini Korea Kusini. Olfati, 24, alizoa alama 14.500 katika fainali ya mashindano hayo ya kibara yaliyofanyika katika jiji la Jecheon nchini Korea Kusini siku ya Jumapili. Hiyo ni medali ya kwanza kabisa ya dhahabu katika historia ya mchezo wa sarakasi kwa Iran katika Mashindano ya Asia.

Mahdi Olfati

 

Raia wa China Huang Mingqi alitwaa medali ya fedha huku Carlos Yulo wa Ufilipino akiambulia medali ya shaba kwa kuzoa pointi 14.400 na 14.333 mtawalia. Olfati, ambaye alikuwa mshindi wa medali ya fedha katika Michezo ya Asia ya Hangzhou ya 2022, alimaliza wa saba kwenye Michezo ya Olimpiki ya Paris ya 2024. Wakati huo huo, Siavash Siahi Kolankouh wa Iran alijishindia medali ya shaba katika Mashindano ya 12 ya Gymnastics ya Kisanaa ya Wanaume ya Asia siku ya Jumamosi. Jumapili ya Juni 8 ilikuwa siku ya mwisho ya Mashindano ya Wanaume ya Asia ya 2025 yaliyoanza Alkhamisi.

Mchujo Kombe la Dunia 2026: Iran yazimwa na Qatar

Timu ya kandanda ya Iran ilishindwa kufurukuta mbele Qatar na kukubali kuzabwa bao 1-0 katika mechi ya mchujo wa kufuzu fainali za Kombe la Dunia la FIFA mwaka 2026.  Katika mechi hiyo iliyopigwa Alkhamisi katika Uwanja wa Jassim Bin Hamad mjini Doha, Iran ilipunguzwa hadi wachezaji 10 katika dakika ya 35 baada ya Milad Mohammadi kupigwa kadi yake ya pili ya njano. Dakika sita baadaye, Pedro Miguel alifanikiwa kucheka na nyavu za wageni. Vijana wa Iran wanaotiwa makali na mkufunzi Amir Ghalenoei walishindwa kusawazisha mechi hiyo.

 

Mchezo wa kwanza wa kocha Julien Lopetegui kuongoza unawafanya Qatar kufikisha pointi 13 katika michezo tisa na kuwaacha wenyeji wa Kombe la Dunia la FIFA 2022 kwa pointi moja nyuma ya Umoja wa Falme za Kiarabu huku mpambano wa Jumanne na Uzbekistan ukisubiriwa kwa hamu. Iran (Kundi A) na Japan (Kundi C) tayari zimethibitisha tiketi zao za fainali za Kombe la Dunia la FIFA mwakani zitakaloandaliwa katika nchi za Canada, Mexico na Marekani.

Magongo; Iran mshindi wa pili

Timu ya mpira wa magongo ya wanawake ya Iran ilizimwa na Ufilipino kwa kulishwa 4-2 katika fainali ya Kombe la Asia la Wanawake la IIHF siku ya Ijumaa na kumaliza katika nafasi ya pili. Iran ilikuwa imeshinda UAE 4-1, India 5-1, Kyrgyzstan 6-0, na Malaysia 6-0 katika michuano hiyo ya kieneo. Timu hiyo ya Iran ilishiriki katika mashindano hayo kwa kuichzesha timu ya vijana. Kombe la Asia la IIHF la Wanawake la 2025 ni mashindano ya kimataifa ya hoki ya barafu ya wanawake yaliyoandaliwa na Shirikisho la Kimataifa la Magongo ya Barafu (IIHF). Michuano hiyo ilifanyika mjini Al Ain, katika Umoja wa Falme za Kiarabu kuanzia Mei 31 hadi Juni 6.

Soka; Tanzania vs Afrika Kusini

Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ilivaana na Bafana Bafana ya Afrika Kusini katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliopigwa kwenye Uwanja wa Peter Mokaba, mjini Polokwane, Afrika Kusini. Mchuano huo wa kirafiki wa kimataifa uliishia kwa sare tasa ya kutofungana. Hata hivyo, mechi hiyo ilijaa mbwembwe za aina yake na mihemko isiyo ya kawaida. Huyu hapa Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, James Bwana akizungumza na wachezaji wa Timu ya Taifa Stars baada ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Afrika Kusini (Bafana Bafana). Ingawa mechi hiyo ilikuwa ya kirafiki, lakini pande zote mbili zimeitumia kama sehemu ya maandalizi muhimu.

 

Kwa Tanzania, mchezo huo ni sehemu ya mikakati ya Kocha Hemed ‘Morocco’ Suleiman katika kuandaa kikosi kwa ajili ya mashindano ya soka ya Afrika CHAN yanayotarajiwa kuanza mwezi Agosti, na pia kuelekea mechi za kufuzu Kombe la Dunia mwezi Septemba. Mchezo huu pia ni sehemu ya maandalizi ya michuano ya CECAFA, huku mashabiki wa soka wakisubiri kuona kiwango cha kikosi hiki kijacho.

Wakati huo huo, timu ya taifa ya Kenya Harambee Stars ililazimishwa sare ya kutofungana na Chad katika mchuano mwingine wa kimataifa wa kirafiki uliopigwa katika mji wa Marakkech nchini Morocco. Mkufunzi wa Harambee, Benny McCarthy, amesema kinachopasa kufanyika sasa ni chinja chinja na kutomhurumia hasimu, baada ya kutoa sare tasa na Chad, huo ukiwa mchezo wa tatu wa kimataifa kwa Kenya ama kushindwa au kuambulia sare chini ya ukufunzi wa raia huyo wa Afrika Kusini.

Fainali, Ligi ya Mataifa ya Ulaya (UEFA); Ureno yaizidi kete Uhispania 

Timu ya taifa ya soka ya Uhispania ilishuka dimbani Jumapilii kuvaana na Ureno katika mchezo wa fainali ya Ligi ya Mataifa ya Ulaya ya UEFA. Ulikuwa mchezo wa kufa kupona, ambapo miamba hiyo ya soka duniani ilitoshana nguvu kwa kutandikana mabao 2-2 katika dakika 90 za ada na za nyongeza, na mwisho wa kwisha wakalizimika kuingia kwenye upigaji matuta. Mabao ya Ureno katika dakika za ada yalifungwa na Nuno Mendes na Cristiano Ronaldo, huku ya Uhispani yakitiwa kimyani na Martin Zubimendi na Mikel Oyarzabal.

Ureno mabingwa wa Ulaya

 

Hatimaye Wareno walitwaa ubingwa baada ya kuibuka kidedea katika upigaji penati, ambapo walifunga mabao 5, huku Wahispania wakitikisa nyavu mara 3. Ufaransa iliitandika Ujerumani mabao 2-0 katika mechi ya kutafuta mshindi watatu kwenye mashindano hayo ya UEFA.

Kwengineko, mwanasoka wa Argentina, Enzo Pittau amefariki dunia baada ya kuanguka uwanjani dakika ya 41 ya kipindi cha kwanza cha mchezo kutokana na mshtuko wa moyo. Kabla ya hayo yote kutokea, alitumia akaunti zake za mitandao ya kijamii kusema kwamba alikuwa amejitolea kila kitu kwa mchezo huu. Baada ya kifo hicho cha ghafla, mechi iliakhirishwa mara moja na usimamizi wa timu ya Don Orione ulionyesha mshikamano wake na mchezaji huyo. Vyombo vya habari vya eneo hilo vinasema Pittau alikuwa amerejea Chaco ili kuwa karibu na familia yake na kumuuguza babu yake ambaye ana matatizo ya kiafya. Katika habari nyingine ya tanzia, mchezaji kandanda kinda wa Kenya, Eric Wafula ameuawa baada ya kupigwa kitutu na umati jijini Nairobi. Wafula ambaye alikuwa kipa wa Mathare FC aliuawa wikendi akiwa pamoja na rafiki yake ambaye hakutajwa jina katika mtaa wa Pangani jijiini Nairobi, baada ya kutuhumiwa kuiba simu ya rununu.

Huku hayo yakijiri, mwanariadha nyota wa Kenya, Beatrice Chebet anaendelea kuimarisha kampeni yake ya kuvunja rekodi za dunia msimu huu. Mshikilizi huyo wa rekodi ya dunia ya mita 10,000 alikimbia kwa mara ya pili kwa kasi zaidi katika historia kwa mara nyingine tena kwenye Ligi ya Diamond ya Rome usiku wa kuamkia Jumamosi, baada ya onyesho lingine la kihistoria kwenye mbio za Rabat mnamo Mei 25. Huko Roma, Chebet—bingwa wa Olimpiki mara mbili aliimarisha umbuji wake katika mbio za mita 5000 na kuibuka kidedea kwa kutumia dakika 14, sekunde 03 nukta 69. Aliwaonyeha kivumbi Mhabeshi Freweyni Hailu aliyeibuka wa pili, huku orodha ya tatu bora ikifungwa na Muitaliano, Nadia Battocletti.

Na mwanakandanda nyota, Ousmane Dembele ni miongoni mwa wachezaji wanaopewa nafasi kubwa ya kushinda taji la Ballon d'Or, baada ya kufunga mabao 33 na kusaidia Paris Saint-Germain kutwaa taji lao la kwanza la Ligi ya Mabingwa Ulaya. Aidha kinda wa Barcelona, Lamine Yamal, naye ni miongoni mwa wachezaji wanaotajwa sana kutokana na kiwango alichoonyesha msimu huu. Nyota mwingine anayetazamiwa kutoa ushindani kwenye tuzo hiyo ya kifahari itakayotolewa Septemba mwaka huu jijini Paris ni Mmisri, Mohammed Salah.

Mmisri, Mohammed Salah

 

Nguli wa Ureno, Cristiano Ronaldo pia anadhani kwamba tuzo ya mwaka huu ya Ballon inapasa kumwendea bamdogo, Lamine Yamal. Wazo hilo linaendana na la nyota wa Real Madrid, Mfaransa, Kylian Mbappe, ambaye anasema tuzo hiyo inapasa kumwendea ama Yamal au Dembele. Kiungo wa Manchester City, Rodri, ndiye mshindi wa tuzo hiyo kwa mwaka uliopita.

………………….MWISHO…..………..