Spoti, Agosti 25
https://parstoday.ir/sw/news/event-i129974-spoti_agosti_25
Natumai u bukheri wa afya hapo ulipo msikilizaji mpenzi. Karibu tuangazie baadhi ya matukio muhimu ya spoti yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita katika pembe mbali mbali za dunia.
(last modified 2025-10-13T11:53:10+00:00 )
Aug 25, 2025 07:15 UTC
  • Spoti, Agosti 25

Natumai u bukheri wa afya hapo ulipo msikilizaji mpenzi. Karibu tuangazie baadhi ya matukio muhimu ya spoti yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita katika pembe mbali mbali za dunia.

Makadeti wa Iran wang'ara

Timu ya judo ya makadeti wa Iran imetawazwa kuwa bingwa wa Kombe la Asia mjini Amman, Jordan, baada ya kupata nafasi ya kwanza katika kitengo cha wavulana na wasichana. Mashindano hayo ya siku mbili yalikamilika Ijumaa usiku mjini Amman, Jordan, huku kikosi cha Iran kikitawala mashindano hayo. Timu hiyo ilinyakua taji la ubingwa wa jumla kwa kujizolea medali tisa: dhahabu nne, fedha tatu na shaba mbili. Katika viwango vya mwisho vya timu, Syria ilimaliza katika nafasi ya pili, ikifuatiwa na Kuwait katika nafasi ya tatu. Samira Khakkhah, Sobhan Hakimi, Abolfazl Nazari, na Yasin Parhizgar walisimama juu ya jukwaa kama washindi wa medali za dhahabu.

 

Medali za fedha zilitunukiwa Hossein Novin, Amirhossein Nazari, na Mohammadreza Kazemi, huku Younes Shabani na Tara Bagheri wakikamilisha hesabu ya medali kwa shaba. Michuano ya Amman Cadet Asian Cup 2025, iliyofanyika Jordan kuanzia Agosti 21 hadi 22, ilishirikisha wanajudo 108 wanaowakilisha nchi 13. Mashindano hayo yanaendelea kwa Kombe la Vijana, ambayo yanapangwa kufanyika kuanzia Agosti 23 hadi 24.

Ligi Kuu ya Soka ya Iran yaanza kurindima

Ligi Kuu ya Soka ya Iran imeendelea kurindima, huku timu zilizoonekana kuwa vibonde katika msiimu uliopita zikianza kwa kasi isiyo ya kawaida. Klabu ya soka ya trekta, washindi wa Ligi ya Ghuba ya Uajemi (PGPL) walishindwa kufurukuta mbele ya Esteghal, mshindi wa Kombe la Hazfi (Mtoano) katika mechi yao ya kwanza ya msimu wa habari wa PGPL Jumanne. Timu ya soka ya Esteghlal ilifanikiwa kupata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya watengeneza matrekta wa Iran katika wiki ya kwanza ya PGPL Jumanne iliyopita. Timu zote mbili zilipoteza fursa kibao za kufunga. Mohammad Hossein Eslami alifunga bao pekee na la ushindi kwenye mchuano huo, katika dakika ya 67. Si vibaya kuashiria hapa kuwa, klabu ya Tractor ilikuwa imeilaza Esteghlal mabao 2-1 mnamo Agosti 11 kwenye mchuano wa Iran Super Cup.

Robo Fainali CHAN

Kenya, Tanzania na Uganda, wenyeji wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) wameyaaga mashindano hayo kiume, baada ya kuondolewa kwenye robofainali kupitia upigaji penati. Atania mwenye kutania, kuwa nchi tatu hizo ni ndugu wa toka nitoke.  Timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars imeungana na Kenya kwenye mlango wa kutokea kwenye michuano ya CHAN 2024 kufuatia kipigo cha 1-0 dhidi ya Morocco kwenye robo fainali ya michuano hiyo katika dimba la Benjamin Mkapa. Morocco imeungana na Madagascar kwenye nusu fainali ya michuano hiyo, Madagascar ikifuzu kufuatia ushindi wa penalti 4-3 dhidi ya wenyeji wenza, Kenya kwenye robo fainali.

Wachezaji wa Taifa Stars uwanjani

 

Taifa Stars, imeondolewa rasmi katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) 2024 baada ya kuchapwa bao 1-0 na Timu ya Taifa ya Morocco katika mchezo wa hatua ya robo fainali uliopigwa leo, Ijumaa, Agosti 22, 2025, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam. Mchezo huo uliokuwa wa ushindani mkubwa na uliohudhuriwa na mashabiki wengi wa soka kutoka ndani na nje ya nchi, ulikuwa wa kipekee kwa Taifa Stars waliokuwa na matumaini ya kuandika historia kwa mara ya kwanza kufuzu hatua ya nusu fainali katika michuano hiyo. Hata hivyo, matumaini hayo yalizimwa na bao pekee lililofungwa na mshambuliaji wa Morocco, Ayoub Lamlioui, katika dakika ya 65 ya kipindi cha pili.

 

Bao hilo lilitokana na shambulizi la kushitukiza lililoanzia katikati ya uwanja, ambapo Lamlioui alimalizia kwa ustadi mkubwa baada ya kupokea pasi murua kutoka kwa kiungo wao mahiri. Tanzania ilijitahidi kurejea mchezoni na kutafuta bao la kusawazisha kwa kufanya mabadiliko kadhaa ya kikosi, likiwemo kuingia kwa washambuliaji wapya ili kuongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji, lakini juhudi hizo hazikuzaa matunda hadi dakika 90 za mchezo kumalizika. Matokeo haya yanamaanisha kuwa Morocco wanafuzu hatua ya nusu fainali ya michuano ya CHAN 2024. Kwa upande wa Tanzania, licha ya kutolewa, wamepongezwa kwa mchezo mzuri na ushindani waliouonesha katika hatua za awali za mashindano, ikiwa ni pamoja na kufuzu kwa hatua ya robo fainali, hatua ambayo haijazoeleka mara kwa mara katika historia ya ushiriki wao wa CHAN. Mashabiki na wadau wa soka nchini wametakiwa kuendelea kuiunga mkono timu hiyo na kuwekeza zaidi kwenye maandalizi ya mashindano yajayo, ikiwa ni pamoja na kufanyia kazi maeneo yaliyoonekana kuwa na mapungufu, hasa katika safu ya ushambuliaji na umakini wa safu ya ulinzi. 

Mashabiki wa Harambee Stars wakifuatilia mikwaju ya penati Kasarani

 

Harambee Stars pia imesukumizwa nje ya michuano ya kombe la Mataifa Afrika kwa wachezaji wa ndani CHAN2024 kufuatia kipigo cha penalti 4-3 dhidi ya Madagascar kwenye mchezo wa robo fainali katika dimba la Moi Sports Centre, Kasarani jijini Nairobi. Mechi iliisha kwa sare ya bao 1-1 katika muda wa kawaida na hata dakika 30 za nyongeza, kabla ya Kenya kushindwa kwenye mikwaju ya penalti, na hivyo kukatiza kampeni ya matumaini ambapo walimaliza bila kushindwa katika hatua ya makundi. Uganda, nchi nyingine mwenyeji wa mashindano hayo ya kikanda, siku ya Jumapili ilishuka dimbani kutupa karata yake ya mwisho. Safari ya Uganda kwenye michuano ya CHAN pia iliishia kwa majonzi katika Uwanja wa Namboole, ambapo bao la Ouma Ba la kipindi cha pili liliwapa mabingwa watetezi Senegal ushindi hafifu wa goli 1-0, na kuzima matumaini ya mwisho ya Afrika Mashariki. Sudan wamesogea mbele kimuujiza, baada ya kuishinda Algeria kwenye upigaji matuta. Hii ni baada ya timu hizo kukabana koo katika mchuano mwingine war obo fainali, ambapo walizabana bao 1-1 katika muda wa ada na dakika 30 za nyongeza. Usidhani tu ni nchi za Afrika Mashariki zimetifulia mavumbi kwenye mashindano hayo ya kibara. Miamba ya soka barani Afrika kama Nigeria, Zambia, DRC, Afrika Kusini zilifungishwa virago kwenye mashindano hayo ya kikanda mapema, baadhi zikishindwa hata kutinga robofainali. Katika mechi zijazo za nusu fainali, Sudan itavaana na Madagascar Jumanne katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, wakati ambapo Morocco watakuwa wanatoana udhia na Senegal katika Uwanja wa Mandela jijini Kampala. Fainali ya mashindano hayo ya kibara itapigwa Jumamosi ijayo katika Uwanja wa Kasarani jijini Nairobi.

 

Riadha: Mkenya awika Diamond League

Mwanariadha Doris Lemngole kutoka Chuo Kikuu cha Alabama nchini Marekani alionja ushindi wake wa kwanza kabisa katika mashindano ya riadha za Diamond League baada ya kuponyoka na taji la mita 3,000 kuruka viunzi na maji, duru ya Lausanne nchini Uswisi, Jumatano usiku. Lemngole, ambaye hakumaliza 3,000m kuruka viunzi na maji mara ya kwanza alishiriki Diamond League wakati wa duru ya Doha nchini Qatar mwezi Mei 2023, alinyakua taji la Lausanne kwa kutumia dakika 9:16.36 na tuzo ya dola 10,000. Kutoka orodha ya washiriki 12, Lemngole alifuatwa kwa karibu na Muethiopia Sembo Almayew (9:20.39) na Mmarekani Olivia Markezich (9:20.73) waliovuna dola 7,000 na Sh 5,000 mtawalia. Mambo hayakuwa mazuri kwa bingwa wa Olimpiki wa 800m, Emmanuel Wanyonyi, aliyeduwazwa na Muingereza Josh Hoey katika mbio hizo za kuzunguka uwanja mara mbili. Hoey alitwaa ubingwa kwa 1:42.82 naye Mhispania Mohamed Attaoui akafunga tatu-bora (1:43.38). Mshindi wa dunia Marco Arop kutoka Canada alikamata nafasi ya tano kutoka orodha ya watimkaji 10 kwa 1:43.91. Mzawa wa Kenya, Isaac Kimeli anayekimbilia Ubelgiji, alitawala 5,000m kwa 13:07.67 akifuatiwa na Mwamerika Grant Fisher (13:08.51) na Eduardo Herrera kutoka Mexico (13:09.50).

Kwengineko, Kenya imetwaa tena taji la mashindano ya shule za upili za Afrika Mashariki. Kenya imeibuka kidedea kwa kuzoa medali 21 za dhahabu, 24 za fedha na shaba 18 kwenye mashindano hayo ya Shirikisho la Michezo ya Shule za Msingi na Sekondari Afrika Mashariki (FEASSA 2025). Uganda imeibuka ya pili kwa kuzoa medali 16 za dhahabu, 15 za fedha na 17 za shaba. Jirani Tanzania pia iling’ara katika mashindano hayo ya kieneo, baada ya kufanya vizuri kwenye michezo ya riadha na kujinyakulia medali nyingi katika fainali zilizofanyika mjini Kakamega, Kenya. Tanzania iliibuka ya tatu huku Rwanda ikimalizia katika nafasi ya nne kwenye mashindano hayo yaliyofanyika mjini Kakagema, magharibi ya Kenya.

Dondoo za Hapa na Pale

Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameipongeza Timu ya Olimpiadi ya Astronomia ya Iran kwa kushinda taji la ubingwa wa dunia kwa mwaka wa pili mfululizo.

Timu ya Olimpiadi ya Astronomia ya Iran

 

Timu ya Iran ilishinda ubingwa wa dunia katika toleo la 18 la Olimpiadi ya Kimataifa ya Astronomia na Astrofizikia (IOAA) huko Mumbai, India, ambapo wanafunzi zaidi ya 300 kutoka shule za upili kutoka nchi 64 walishindana. Timu ya Iran imeweza kupata medali tano za dhahabu katika mashindano hayo yaliyofanyika Agosti 11 hadi 21 mwaka huu.

Katika hatua nyingine, kuelekea mchezo muhimu wa kuwania kufuzu kwa Kombe la Dunia kwa Italia dhidi ya Israel, Chama cha Makocha wa Italia (AIAC), pia kinachojulikana kama Assoallenatori, kimezitaka rasmi shirikisho la soka la kimataifa kusimamisha Israel kushiriki mashindano ya kimataifa ya kandanda. Katika barua iliyotumwa kwa Rais wa Shirikisho la Soka la Italia (FIGC) Gabriele Gravina, AIAC ilisema rufaa yao si ya kiishara tu bali ni "chaguo la lazima" linaloendeshwa na "lazima ya kimaadili." Barua hiyo, iliyoripotiwa na vyombo vya habari vya Italia na kumnukuu rais wa AIAC Renzo Ulivieri, inaonyesha uamuzi wa pamoja wa bodi ya kitaifa ya chama hicho.

 

"Maadili ya ubinadamu, ambayo ni msingi wa yale ya michezo, yanatulazimisha kupinga vitendo vya ukandamizaji na matokeo mabaya," Ulivieri anasema, akihutubia Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) na Muungano wa Vyama vya Soka vya Ulaya (UEFA).  

Huku hayo yakijiri, mchezaji mwingine wa soka Palestina ameuawa shahidi na jeshi la utawala ghasibu wa Israel akiwa katika safu ya chakula cha msaada huku Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) likiendelea kukaa kimya. Vyanzo vya habari viliripoti kuuawa shahidi mmoja wa wachezaji wa timu ya soka ya Al-Jazeera wakati wa mashambulizi ya utawala wa Israel dhidi ya foleni ya kusubiria chakula cha msaada kaskazini mwa Gaza. Vyanzo vya habari vilitangaza kuwa Muhannad Jamal Alian, mchezaji wa timu ya soka ya Al-Jazeera, ameuawa shahidi kaskazini mwa Ukanda wa Gaza. Duru hizo pia zimetangaza kuwa, mwanasoka huyo kijana wa Kipalestina pamoja na raia wengine wa Palestina walikuwa wamesimama kwenye foleni wakisubiri kupokea misaada ya kibinadamu wakati alipolengwa na utawala wa Israel katika kaskazini mwa Ukanda wa Gaza na kuuawa shahidi. Hivi karibuni nahodha na nyota wa zamani wa timu ya taifa ya Palestina Suleiman al-Obeid, anayejulikana kama Pele wa soka ya Palestina aliuawa shahidi katika shambulizi la kinyama la utawala wa kizayuni wa Israel alipokuwa akisubiri msaada wa chakula huko Gaza. Francesca Albanese, Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kufukuzwa timu za michezo za utawala wa Kizayuni katika mashindano ya kimataifa. Katika miezi ya hivi karibuni, utawala wa Kizayuni kwa kutumia kisingizio cha "utaratibu wa kutoa misaada ya kibinadamu" uliobuniwa na Marekani kwa ushirikiano wa Tel Aviv, umewaelekeza Wapalestina masikini katika maeneo maalumu ya Ukanda wa Gaza na kisha kuwafyatulia risasi na kulipua mabomu kwa mpangilio.

Kwengineko, Emamali Habib, mshindi wa kwanza wa medali ya dhahabu wa Iran katika Michezo ya Olimpiki, alifariki dunia siku ya Jumapili. Alikufa huko Sari, Mkoa wa Mazandaran, baada ya kusumbuliwa na ugonjwa wa muda mrefu. Habibi alishinda medali ya kwanza ya dhahabu ya Iran katika historia katika Michezo ya Olimpiki ya 1956.

Marehemu Emamali Habib

 

Mwanamieleka huyo wa freestyle, aliyepewa jina la utani la Tiger of Mazandaran, alifariki akiwa na umri wa miaka 94. Habibi pia alishinda medali tatu za dhahabu katika 1959, 1961, na 1962 World Wrestling Championships.

Mbali na hayo, mechi ya ya Ngao ya Jamii (Community Shield) ya kuizindua msimu mpya wa Ligi Kuu kati ya Young Africans na Simba itachezwa Septemba 16, 2025 jijini Dar es Salaam. Kwa mujibu wa TFF, Mfumo wa mashindano ya Ngao ya Jamii umebadilika kutokana na marekebisho ya kanuni yaliyopitishwa katika kikao kilichopita cha Kamati ya Utendaji ya TFF.

Na katika Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza, Arsenal iliichabaganga Leeds mabao 5-0 Jumamosi katika mchezo ambao klabu hiyo ilimshirikisha kinda, Max Dowman mwenye umri wa miaka 15. Gunners wana imani kubwa kwamba wamempata lulu mpya. Uchezaji wake wa kwanza tayari umeandika jina lake kwenye historia ya klabu na huenda ikawa mwanzo wa safari ndefu yenye mafanikio katika klabu hiyo ya kaskazini mwa London. Watani wa Wabeba Bunduki, klabu ya Machester United walilazimishwa sare ya bao 1-1 na Fulham, wakati ambapo Everton ilikuwa inainyuka Brighton mabao 2-0.

………………..TAMATI…………….