Ulimwengu wa Spoti, Sep 15
https://parstoday.ir/sw/news/event-i130840-ulimwengu_wa_spoti_sep_15
Natumai u mzima wa afya mpenzi msikilizaji popote pale ulipo. Karibu tuangazie baadhi ya matukio muhimu ya spoti yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita katika pembe mbali mbali za dunia.
(last modified 2025-10-17T05:53:46+00:00 )
Sep 15, 2025 11:38 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Sep 15

Natumai u mzima wa afya mpenzi msikilizaji popote pale ulipo. Karibu tuangazie baadhi ya matukio muhimu ya spoti yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita katika pembe mbali mbali za dunia.

Voliboli: Iran yaduwazwa na Misri

Iran imeanza vibaya mashindano ya kimataifa ya voliboli nchini Ufilipino, licha ya kuitandika Ujerumani alama 3-1 (25-20, 20-25, 25-23, 26-24) katika mechi ya kirafiki ya kujiandaa kwa Mashindano ya Dunia ya Wanaume 2025. Misri iliifunga Iran alama 3-1 (25-17, 16-25, 25-23, 25-20) katika siku ya tatu ya Mashindano ya Dunia ya Voliboli ya Wanaume ya FIVB ya 2025 Jumapili. Iran ilishindwa kufurukuta mbele ya Mafarao, ambapo Ahmed Shafik aliiongoza Misri kwa pointi 18, wakati Ali Hajipour akikusanyia Iran pointi 17.

Iran na Misri zikipambana uwanjani

 

Iran ipo katika Kundi A pamoja na Misri, Tunisia na Ufilipino. Imeratibiwa kuvaana na Tunisia na Ufilipino siku za Jumanne na Alkhamisi mtawalia jijini Manila. Timu 32 kutoka kote duniani zinachuana kuwania taji hilo la kifahari. Zimegawanywa katika makundi manane, kila kundi likiwa na timu nne, ambapo mbili za kwanza zitafuzu hatua ya mtoano. Michuano hiyo inayopigwa katika kumbi za michezo za SM Mall Asia Arena na Smart Araneta Coliseum huko Manila, inatamatika 28 Septemba, ambapo fainali itaamua ikiwa Italia itatetea taji lao au mabingwa wapya wataibuka.

Majudoka wa Iran wazoa medali Indonesia

Mabingwa wa judo wa Iran wameshinda medali moja ya fedha na mbili za shaba katika Mashindano ya Judo ya Asia yaliyofanyika Jakarta, mji mkuu wa Indonesia. Katika pambano la Ijumaa usiku, Muirani, Samira Khak-khah aliibuka wa pili katika kitengo cha mabanati walio na chini ya kilo 63. Aliwabwaga wapinzani kutoka Jordan na Indonesia na kutinga fainali, ambapo alikabiliana na mshindani mkali kutoka Korea Kusini. Licha ya juhudi zake, Khak-khah alipoteza mechi hiyo muhimu, na kuishia kutwaa medali ya fedha. Katika safu ya majudoka wa kiume, Amirhossein Nazari alinyakua medali ya shaba katika kategoria ya uzani wa chini ya kilo 90. Aidha Mohammad Pouria Banaeian alishinda shaba baada ya kumlemea raia mwenza Ali-Asghar Malekzadeh katika pambano la kuwania nafasi ya 3.

Mieleka: Zare ashinda dhahabu Croatia

Amirhossein Zare wa Iran, mwanamieleka wa uzani wa juu, alishinda medali ya dhahabu katika Mashindano ya Dunia ya Mieleka ya 2025 siku ya Jumapili. Zare ilimshinda Giorgi Meshvildishvili wa Azerbaijan 5-0 katika pambano la mwisho la kilo 125. Alikuwa ameshinda Jonovan Smith wa Puerto Rico 11-0, Solomon Manashvili wa Georgia 10-0, na Shamil Sharipov wa Bahrain 7-0 akielekea fainali. Robert Baran wa Poland na Sharipov walishinda medali za shaba. Wakati huo huo, mwanamieleka muingine wa Iran, Ahmad Javan alishinda medali ya fedha Jumapili baada ya kuzidiwa kete na Zaur Uguev 11-2 katika pambano la fainali la wanamieleka wenye kilo 61.

 

Naye Kamran Ghasempour alinyakua medali ya shaba katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu siku ya Jumapili. Hii ni baada ya kumpeleka mchakamchaka mwanamieleka wa India Mukul Dahiya na kumshinda kwa alama 10-0 katika mchezo huo. Mashindano ya Dunia ya Mieleka ya 2025 yanayofanyika Zagreb, Croatia tangu Septemba 13, yanatazamiwa kufunga pazia lake Septemba 21.

Riadha: Kenya yang'ara Japan

Mwanariadha nyota wa Kenya, Beatrice Chebet aliishindia nchi yake medali ya kwanza ya dhahabu katika Mashindano ya Riadha ya Dunia huyo Tokyo, Japan, na kufungua mlango wa medali zaidi. Bingwa huyo mara mbili wa Olimpiki aliibuke kidedea kwa kutumia dakika 30 na sekunde 37.61, kushinda fainali ya mita 10,000 kwa wanawake mbele ya Nadia Battocletti wa Italia. Chebet alitimka kama risasi zikiwa zimesalia mita 200, akiwatifulia mavumbi Battocletti, Mhabeshi Gudaf Tsegay na raia mwenza Agnes Ng'etich. Chebet sasa anatazamiwa kuwania medali dhahabu katikambio za mita 5000 baadaye katika mashindano hayo. Dhahabu nyingine ya Kenya ilitwaliwa na mwanadada Peres Jepchirchir katika mbio za marathoni siku ya Jumapili.

Peres Jepchirchir aishindia Kenya dhahabu ya 2 Tokyo

 

Alitumia saa 2, dakika 24 na sekunde 43 kumaliza mbio hizo za kilomita 42, mbele ya Mhabeshi Tigst Assefa, huku Julia Patternain wa Uruguay akikamilsiha orodha ya tatu bora. Duru ya 20 ya Mashindano ya Riadha ya Dunia yalianza Jumamosi mjini Tokyo, Japan, huku zaidi ya wanariadha 2,000 kutoka takriban nchi 200 dunia wakipambana kufa kupona kushinda medali na kuyaheshimisha mataifa yao.

Simba Day; Wekundu wainyuka Gor

Tamasha la Simba Day 2025 limehitimishwa kwa mchezo wa kirafiki wa kimataifa kati Wekundu wa Msimbazi, Simba SC ya Tanzania dhidi ya Gor Mahia ya Kenya. Mchezo huo wa kirafiki ulipigwa Septemba 10, ambapo Simba SC ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Gor Mahia, mchezo ambao ulihitimisha sherehe za Simba Day 2025 katika Uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam. Mbao ya Simba SC yalifungwa na Abdulrazak Hamza dakika ya sita ya mchezo na Steven Desse Mukwala dakika ya 65 na kufanikiwa kupata ushindi katika mchezo huo muhimu. Watani wa jadi wa Simba, klabu ya Yanga siku ya Jumamosi pia waliadhimisha Yanga Day kwa mbwembwe za aina yake jijini Dar es Salaam.

Mashabiki wa Simba Tanzania

 

Siku ya Mwananchi ilinogeshwa na kichapo cha bao moja kwa nunge, dhidi ya Bandari FC ya Kenya. Nyota mpya wa Yanga, Celestin Ecua raia wa Chad ndiye aliyefunga goli pekee lililowapa ushindi wa 1-0 dhidi ya Bandari katika mchezo wa kirafiki kuhitimisha sherehe za Kilele cha Wiki ya Mwananchi kwenye Dimba la Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Soka la Wanawake Afrika; Nusu Fainali Cecafa

Michuano ya nusu fainali za Kipute cha Kufuzu Mashindano ya Shirikisho la Soka Afrika Mashariki Cecafa yatakayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrka CAF imechezwa Jumapili hii ya Septemba 14, katika Uwanja wa Kasarani jijini Nairobi, Kenya.  Matumaini ya timu ya Kenya Police Bullets kutinga fainali ya kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa wa CECAFA ya Wanawake yalimalizika kwa huzuni baada ya kulazwa kwa penalti 4-2 na JKT Queens ya Tanzania katika mchuano mkali uliochezwa kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Michezo wa Moi, Kasarani, Jumamosi.

Timu za CECAFA

 

Bullets walianza kwa nguvu, walichukua uongozi katika dakika ya 18 wakati fowadi wa Uganda Margaret Kunihira alifunga kwa utulivu mkwaju wa penalti uliopigwa na Emily Kemunto Morang’a. Wakiwa wameweka pasi safi katika muda wote wa michuano hiyo, hili lilikuwa bao la kwanza kufungwa na JKT. JKT Queens imetinga fainali mzima mzima, ambapo Jumanne hii ya Septemba 16 itamenyana na Rayons ya Rwanda, ambayo awali iliichabanga Kampala Queens ya Uganda mabaoa 4-3 kupitia upigaji matatu, kwenye nusu fainali ya kwanza ya kuwania tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa ya CAF.

Dondoo za Hapa na Pale

Mbunge mmoja kutoka Scotland amewasilisha hoja rasmi akitaka mashirika ya michezo barani Ulaya kuiondoa Israel katika mashindano ya kimataifa kutokana na mauaji ya kimbari yanayoendelea huko Gaza. Hoja hiyo, iliyowasilishwa katika Bunge la Uskochi na James Dornan, ililaani uanachama wa Israel katika vyama vya michezo vya Ulaya, ikizitaka taasisi husika kufuta ushiriki wake mara moja. Dornan amezitaka taasisi kama vile Shirikisho la Soka la Ulaya (UEFA), Shirikisho la Mpira wa Kikapu Ulaya, Shirikisho la Mpira wa Mikono Ulaya, na Shirikisho la Riadha Ulaya kuchukua hatua ya haraka ya kuiondoa Israel.

 

Mwezi uliopita pia, Francesca Albanese, Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu katika maeneo ya Palestina, alitoa wito kwa UEFA kuifukuza Israel kutoka mashindano kwa kuwa utawala huo umehusika katika uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu katika Ukanda wa Gaza.

Mbali na hayo, klabu ya Manchester United iligeuzwa kichwa cha mwendawazimu katika debi la London, baada ya kunyolewa bila huruma na watani wao, Manchester City. City wakiiupigia nyumbani Etihad, waliwabamiza Mashetani Wekundu mabao 3-0, na kuwafanya waondoke uwanjani wakiwa wamenywea, vichwa chini, mikono nyuma. Bao la kwanza la City lilitiwa kimyani na Phil Foden kunako dakika ya 18, huku nyota Erling Haaland akicheka na nyavu mara mbili kipindi cha pili, katika dakika za 53 na 68. Aidha Liverpool iliitandika Burnley bao moja la uchungu bila jibu katika mchezo mwingine wa wikendi wa Ligi Kuu ya Uingereza, na kutuama kileleni mwa jedwali wakiwa na alama 12. Arsenal pia iliiishikua vibaya Nottinmgham Forest kwa kuisasambua mabao 3-0. Wakiupigia nyumbani katika Uwaja wa Emirates, Wabeba Bunduki waliutawala mchezo, ambapo Martin Zubimendi alifunga mawili katika dakika za 32 na 79, huku Viktor Gyokores akipigilia msumari wa mwisho kwenye jeneza la wanamisitu. Gunners kwa sasa wanaridhika na nafasi ya pili wakiwa na alama 9, wakibebwa na Tottenham ambao pia wana alama 9.

Na tunatamatisha kwa habari ya tanzia, ambapo mwanamasumbwi bingwa wa zamani wa dunia Ricky Hatton amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 46, wiki chache tu baada ya kutangaza kurejea ulingoni. Kwa mujibu wa  gazeti la Daily Mail, mzawa huyo wa jiji la Manchester alipatikana amepoteza maisha nyumbani kwake huko Greater Manchester Jumapili hii ya Septemba 14. Mamlaka za Uingereza zimethibitisha kuwa kifo chake hakichukuliwi kama cha kutiliwa shaka.

……………………MWISHO………………