EID GHADIR NA KUMBUKUMBU YA KUAGA DUNIA IMAM KHOMEINI (Mwenyezi Mungu Amrehemu)
-
Eid Ghadir na Kumbukumbu ya Kuaga Dunia Imam Khomeini (M.A)
Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Hamdu zote ni za Mwenyezi Mungu aliyetujaalia kuwa miongoni mwa wanaoshikamana na Wilaya ya Amirul Muuminin, Ali bin Abi Talib AS.
Tarehe 17 ya mwezi wa Mfunguo Tatu, Dhul Hijjah ni siku ya Idi ya Wilaya, maarufu kama Idi ya Ghadir-Khum, ya utawala wa Uimamu ulioainishwa na Mwenyezi Mungu; siku ambayo Yeye Mola Mwenye Enzi alitukamilishia dini Yake na akauchagua Uislamu kuwa dini iliyokamilika kwa ajili ya wanadamu wote.
Kilichoifanya dini iwe imekamilika katika siku hiyo ni hukumu na amri ya Mwenyezi Mungu, ambayo kama ulivyo uzi wa tasbihi iliziunganisha pamoja hukumu nyingine zote za Uislamu. Katika kipindi cha miaka ishirini na mitatu ya Utume wa Mtume wa Mwisho, Nabii Muhammad Al-Mustafa SAW, Mwenyezi Mungu Tabaaraka Wa Taala aliteremsha hukumu mbalimbali za Uislamu moja baada ya nyingine; kuhusu vyakula na vinywaji, kuhusu jirani, Mtume wake na watu, kuhusu Sala, biashara, Jihadi na nyanja nyingine nyingi za maisha ya watu.
Hadi wakati huo, aliyekuwa akiunganisha na kuzifafanua hukumu zote hizo ni Bwana Mtume SAW mwenyewe. Katika mazingira magumu ya dhiki na ya mbinyo wa hali binafsi na ya kijamii, yeye ndiye aliyekuwa akiwabainishia watu hukumu za dini; na sira na mwenendo wake vilikuwa ruwaza na kigezo cha kufuatwa ili kuweza kutambua na kupambanua yaliyo sahihi na ya upotofu. Hata hivyo, baada ya miaka ishirini na mitatu ya Utume, ukawadia wakati ambapo Mtume wa Allah ilibidi atawafu na kutengana na Waislamu moja kwa moja ili kuelekea kwenye ulimwengu wa malakuti, wa rehma za Mwenyezi Mungu, wa maisha ya milele. Kulikuwepo na hofu kwamba baada ya kuondoka Bwana Mtume SAW, mfumo wa hukumu za Uislamu ungeyumba, na kwa mara nyingine tena ujahilia ungewarejesha watu kwenye lindi la giza la dhalala na upotofu…
Ulikuwa wakati wa msimu wa Hija; na huku Mtume wa mwisho wa Allah akiwa amechanganyika na umati mkubwa wa Waislamu katika kufanya t’awafu, alikuwa akitafakari na kuwaza: Umma wangu utafanya nini baada yangu? Ni katika hali hiyo, ndipo Malaika Jibril akateremka na kumfikishia ujumbe wa Mwenyezi Mungu usemao:
يَٰٓأَيُّهَا ٱلرَّسُولُ بَلِّغۡ مَآ أُنزِلَ إِلَيۡكَ مِن رَّبِّكَۖ وَإِن لَّمۡ تَفۡعَلۡ فَمَا بَلَّغۡتَ رِسَالَتَهُۥۚ
Ewe Mtume! Fikisha uliyo teremshiwa kutoka kwa Mola wako Mlezi. Na ikiwa hukufanya hayo basi hukufikisha ujumbe wake...
Ujumbe huo ambao ufikishaji wake ulitiliwa mkazo na Mwenyezi Mungu kwa kuonyesha kwamba endapo Mtume hatoufikisha, hatokuwa amefikisha itakiwavyo risala ya Utume wake, ulihusu hukumu ambayo kuwepo kwake baada ya hapo kutakuwa sawa na uzi unaounganisha tasbihi za hukumu zote za Uislamu. Ni kiungo madhubuti ambacho kingeifanya Qur’ani, -Kitabu hicho cha mbinguni-, kiendelee kuwa hai milele; tena si kwa hali yake ya dhahiri tu, bali kwa hakika yake kamili ya kimaana kama ilivyoteremshwa kutoka mbinguni. Na kama Yeye Mwenyezi Mungu pekee, ndiye aliyejua ni wapi pa kuiweka risala Yake ya Wahyi, ni Yeye tu pia, ndiye anayejua ni nani anastahiki kurithi nafasi ya Mtume Wake.
Hija ilikuwa imemalizika, na mahujaji wakawa wanaondoka kurejea makwao. Wakati msafara wa Mtume wa Allah ulipofika eneo la Ghadir Khum, Bwana Mtume SAW aliwakusanya Masahaba wote mahala hapo kwa kusema: “Waambieni walioondoka warudi na wale ambao hawajafika, wajihimu kufika haraka”.
Kulikuwa na habari kubwa iliyokuwa inasubiri kutangazwa; habari yenye uzito sawa na juhudi zote za miaka 23 alizofanya Bwana Mtume Muhammad SAW katika kufikisha risala na ujumbe wa Mwenyezi Mungu.
Mimbari ilitengenezwa kwa kutumia matandiko ya ngamia na soji za farasi, na yeye Bwana Mtume akapanda juu yake. Kisha akamwita Ali bin Abi Talib na kumsimamisha kando yake. Baada ya kumhimidi na kumshukuru Mwenyezi Mungu aliushika na kuuinua juu mkono wa Ali na kusema:
"Enyi watu! Hadi sasa sijawahi kukhini chochote katika kufikisha yale niliyoteremshiwa, na hivi sasa pia sitafanya hivyo. Tambueni kuwa, Jibril ameniteremkia mara tatu akiwa ameleta amri itokayo kwa Mola wangu, akiniamuru nisimame mahala hapa, na kuwatangazia watu wote weupe na weusi kwamba Ali bin Abi Talib ni ndugu yangu, wasii wangu, khalifa wangu kwa umati wangu na Imamu baada yangu. Nafasi yake yeye kwangu mimi ni kama ilivyo nafasi ya Harun kwa Musa, kwa tofauti tu kwamba, hakutakuwa na Mtume baada yangu. Baada ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, huyu Ali ndiye mwenye mamlaka juu yenu..."
Wapenzi wasikilizaji, hakika ya Uislamu haiwezi katu kuendana wala kuwekwa mahala pamoja na khulka ya uchu wa kutotosheka na ya kupenda makuu na ukubwa. Uislamu wa kweli uko mbali kabisa na ufisadi na utashi wa hawaa na matamanio ya nafsi. Hakika ya Uislamu haina hata chembe ya uhusiano na ukatili na ulimbikizaji wa mali. Hakika na ukweli huu ulishuhudiwa katika miaka yote ya baada ya kuondoka duniani Bwana Mtume SAW, katika maisha, sira na mafundisho ya Amirul Muuminin Ali AS na Maimamu waliofuatia baada yake wa kizazi cha Bwana Mtume. Na hili ndilo jambo hasa tunalolifuatilia na kulipigania katika dunia ya leo.
Ilikuwa takribani miaka 55 nyuma, wakati Imam Khomeini alipokipata kipoteo hicho kutoka kwenye mafundisho na hukumu kadhaa za Uislamu na akakishika na kukiinua kwa nguvu zake zote. Kipoteo hicho kilikuwa si kingine ila ni nadharia ya Wilayatul-Faqih (yaani Utawala wa Faqihi). Ni Wilaya na utawala ambao ulianza kwa Uimamu wa Ali bin Abi Talib AS, katika siku ya Ghadir; na baada ya kupita vipindi vingi vya dhoruba na shwari, leo hii, katika zama za kughibu Imam Maasumu kimefikia mikononi mwa Faqihi mwadilifu, shujaa na muelewa wa zama.
Imam Khomeini (MA), yeye alikuwa faqihi wa kwanza aliyeshika hatamu za uongozi wa Waislamu kwa niaba ya Imam Maasumu, akainua na kupeperusha bendera ya haki na uadilifu na kupambana na dhulma na ukandamizaji wa madola ya kibeberu ya zama zake.
Katika hotuba yake ya mwisho aliyotoa kuhusu Eid Ghadir, mwasisi huyo wa Jamhuri ya Kiislamu alisema:
"Si tukio la Ghadir ambalo liliinua hadhi ya Ali AS, bali ni kinyume chake; ni adhama ya shakhsia ya Ali AS ndio iliyolifanya tukio la Ghadir liwe la kihistoria… Baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, Ali bin Abi Talib ndiye mtu pekee ambaye alistahiki kusimamisha uadilifu katika jamii kwa namna anavyotaka Mwenyezi Mungu. Kwa sababu hiyo, Mwenyezi Mungu alimteua kuwa kiongozi wa jamii ya Kiislamu, na yote hayo yalitokana na daraja ya kimaanawi ya Amirul-Muuminin Ali AS ".
Kwa mtazamo wa Imam Khomeini, suala la Ghadir halikuwa suala la utawala tu na madaraka ya kidunia, bali lilikuwa suala la kusimamia “uadilifu”. Imam Ali AS aliwahi mara kadhaa kuashiria katika khutba zake kuhusu namna dunia isivyo na thamani. Kwake yeye, dunia ilikuwa duni zaidi kuliko viatu vilivyoshonewa viraka. Kama ni hivyo, itawezekanaje kwa mtu anayeichukulia dunia kuwa duni kiasi hicho, apiganie madaraka ya dunia na kupenda ukubwa? Kwake yeye uongozi na Khilafa vilikuwa na lengo moja tu, ambalo ni kusimamisha uadilifu, ikiwa ndio sababu ya kubaathiwa na kutumwa Mitume wote.
Kwa mtazamo wa Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran aliyeuawa shahidi, katika tukio la Ghadir, mbali na wanavyoitakidi Waislamu wa Kishia kuhusu kuteuliwa Ali AS na Bwana Mtume SAW kuwa kiongozi wa Waislamu, kuna suala jengine muhimu katika tukio hilo ambalo ni: “Msingi wa Wilaya” au utawala. Suala ambalo ikiwa leo hii Waislamu duniani na wananchi wa mataifa ya Kiislamu watalielewa barabara na kwa usahihi wake na wakaungana pamoja na kushikamana nalo kisawasawa, matatizo mengi yanayoutatiza Umma wa Kiislamu yatatatuliwa.
Ili kuuelewa vizuri zaidi ukweli huu, inatakiwa tuizingatie nukta hii, kwamba katika mafundisho ya Qur'ani kuna aina mbili za Wilaya au utawala: “Wilaya ya Haki” na “Wilaya ya Taghuti” au “Utawala wa Shetani”. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema katika Aya ya 257 ya Suratul-Baqarah:
"Mwenyezi Mungu ni Mtawala wa walio amini. Huwatoa gizani na kuwaingiza kwenye nuru. Lakini walio kufuru, watawala wao ni Mashet'ani. Huwatoa kwenye nuru na kuwaingiza gizani. Hao ndio watu wa Motoni, wao watadumu humo ".
Aya hii inabainisha wazi umuhimu wa kulifahamu suala la “Wilaya” au utawala na jinsi linavyohusiana moja kwa moja na hatima ya wanadamu.
Kimsingi watu wote huwa wanaishi kwenye jamii; na jamii hiyo inakuwa na mtawala na mwendeshaji mambo. Mtawala huyo ndiye anayekuwa na mamlaka ya juu kabisa kwa watu wote wa jamii hiyo. Kwa hiyo katika maisha yetu, hakuna mtu yeyote asiye na walii anayemtawalia mambo yake. Ikiwa mtu hataikubali Wilaya ya Walii wa Haki, basi ataangukia katika Wilaya ya Taghuti na kupotea njia. Huenda ni kwa sababu hiyo ndipo Imam Muhammad Al-Baqir AS akasema:
"Uislamu umejengwa juu ya nguzo tano: Sala, Zaka, Saumu ya Ramadhani, Kuzuru Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu na Wilaya ya Maimamu Maasumu". Ikiwa haitakuwepo Wilaya hakuna hata moja kati ya hukumu nyingine za Uislamu itakayoweza kubaki na uimara wake.
Suala la utawala na Wilaya ndilo suala muhimu zaidi na hasasi zaidi kwa kila taifa. Na ndio maana, wakati Shahidi Ayatullah Sayyid Ali Khamenei alipotuma ujumbe kwa Kongamano la Umoja wa Kiislamu la mwaka 1974, aliwahutubu watawala wa baadhi ya nchi za Kiislamu kwa kuwaambia: "Nasaha zetu kwa watawala wa nchi za Kiislamu ni kwamba warejee kwenye Wilaya ya Uislamu; wawe chini ya Wilayatu-Llah. Wilaya ya Marekani na Wilaya ya Taghuti haitawafalia kitu."
Leo, tukiwa katika kumbukumbu ya mwaka wa 37 tangu alipofariki dunia Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu Amrehemu), ukweli huu umewadhihirikia wazi wananchi wa mataifa na tawala za Kiarabu za eneo hili: ya kwamba kuikubali Wilaya na kutawaliwa mambo yao na Shetani Mkubwa Marekani hakujawaletea wao faida yoyote. Shetani huyo anafikiria manufaa yake mwenyewe tu; na kama italazimu atawatoa kafara watu wote ili kufikia malengo yake. Kwa hiyo, acheni kumfuata Shetani na rejeeni kwenye Wilayatu-Llah”.
Wapenzi wasikilizaji, na hasa wa Umma wa Kiislamu duniani kote, Mwenyezi Mungu SWT anatuuliza katika Aya ya 16 ya Suratul-Hadiid: "Je, bado haujafika wakati kwa walioamini kunyenyekea nyoyo zao kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu…?" Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/