Jumatano, tarehe 17 Juni, 2026
-
Leo katika Historia
Leo ni Jumatano tarehe 02 Mfunguo Nne Muharram 1448 Hijria sawa na Juni 17 mwaka 2026.
Siku kama ya leo miaka 1387 iliyopita yaani tarehe Pili Muharram mwaka 61 Hijria Imam Hussein (AS) mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) akiwa pamoja na familia yake, waliwasili katika ardhi ya Karbala katika Iraq ya leo.
Miezi kadhaa kabla ya hapo, Imam Hussein AS aliondoka katika mji mtakatifu wa Madina na kuelekea Makka akilalamikia utawala wa kimabavu wa Yazid bin Muawiya na baadaye akaelekea katika mji wa Kufa huko Iraq.
Japokuwa watu wa Kufa mwanzoni waliunga mkono mapambano ya Imam Hussein na kumwalika katika mji huo, lakini waliacha kumuunga mkono mjukuu huyo wa Mtume kutokana na hofu na vitisho vya utawala wa Yazid bin Muawiya.
Jeshi la Yazidi mlaaniwa liliuzuia msafara wa mjukuu huyo wa Mtume (SAW) kuingia katika mji wa Kufa na kuuzingira katika jangwa na Karbala. *****
Katika siku kama hii ya leo miaka 101 iliyopita sawa na tarehe 17 Juni 1925, ulitiwa saini mkataba wa kupiga marufuku matumizi ya silaha za vijidudu na kemikali mjini Geneva Uswisi.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, utumiaji vitani wa aina yoyote ya silaha za vijidudu, gesi zinazoua, sumu za kemikali na nyinginezo kama hizo ulipigwa marufuku. Licha ya kufikiwa makubaliano hayo, lakini baadhi ya nchi bado ziliendelea kutumia silaha hizo zilizopigwa marufuku duniani.
Ujerumani ilitumia silaha za kemikali katika Vita vya Kwanza vya Dunia, Marekani katika vita vya Vietnam na utawala wa zamani wa Iraq ilitumia silaha hizo wakati wa vita vyake vya kichokozi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. ****
Katika siku kama ya leo miaka 82 iliyopita, wakazi wa kisiwa cha Iceland walifanikiwa kupata uhuru wao kutoka mikononi mwa Denmark.
Kisiwa cha Iceland kiligunduliwa tarehe 10 Julai 874 Miladia na kuanzia wakati huo, ndipo wahajiri wa Norway, Scotland na Ireland wakaanza kuishi katika kisiwa hicho. Hadi kufikia karne ya 13 Miladia ilikuwa ni nchi huru hata hivyo muda baadaye iliunganishwa na Norway na kisha Denmark. Mwaka 1874 Denmark iliruhusu kuundwa baraza la watunga sheria (yaani bunge) katika kisiwa hicho cha Iceland.
Aidha serikali ya ndani ya kisiwa hicho iliendelea kufuatilia haki zake zaidi ingawa bado kiliendelea kutambuliwa kuwa sehemu ya Denmark, hadi tarehe 17 Juni 1944 ambapo kulitangazwa kuvunjwa muungano huo baada ya kurejelewa maoni ya wakazi wa Iceland. Kuanzia wakati huo, wakakazi wa Iceland wanaitambua siku kama ya leo kuwa siku ya kitaifa. ***
Siku kama ya leo miaka 47 iliyopita, yaani tarehe 27 Khordad kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani ya Hijria Shamsia, Imam Khomeini, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitoa amri ya kuasisiwa taasisi ya Jihadi ya Ujenzi kwa ajili ya kulinda uhuru wa Iran, kujitegemea na kumaliza umaskini hususan katika maeneo ya vijijini.
Kufuatia kutolewa amri hiyo, wananchi wa matabaka mbalimbali hasa wanafunzi na wanachuo, vijana wenye ghera na imani na wasomi walijitolea kwenda kufanya kazi za ujenzi za kuwasaidia watu maskini katika pembe mbalimbali za Iran.
Taasisi ya Jihadi ya Ujenzi imezaliwa kutoka ndani ya Mapinduzi ya Kiislamu na hadi sasa inafanya kazi kubwa za ujenzi na kusaidia watu maskini na wenye haja. Taasisi hiyo inajihusisha na mambo mengi yakiwemo masuala ya viwanda, kazi za vijijini, kilimo, ufugaji, ujenzi wa mabwawa, kulinda mazingira na makumi ya kazi nyingine za kujenga taifa.
Mwaka 1362 Hijria Shamsia Taasisi ya Jihadi ya Ujenzi ya Iran ilibadilishwa na kuwa Wizara, na mwaka 1379 Hijria Shamsia iliingizwa kwenye Wizara ya Kilimo ya Iran. ***