“Hormuz, Lango Takatifu”
https://parstoday.ir/sw/news/event-i139208-hormuz_lango_takatifu
Matumaini yangu mpenzi msikilizaji ni kuwa hujambo popote pale ulipo. Karibu kuwa pamoja nami katika makala yetu ya wiki hii yenye anuani: “Hormuz, Lango Takatifu”.
(last modified 2026-06-17T07:31:22+00:00 )
Jun 17, 2026 07:20 UTC
  • Mlango- Bahari wa Hormuz
    Mlango- Bahari wa Hormuz

Matumaini yangu mpenzi msikilizaji ni kuwa hujambo popote pale ulipo. Karibu kuwa pamoja nami katika makala yetu ya wiki hii yenye anuani: “Hormuz, Lango Takatifu”.

Baadhi ya vivuko na njia za baharini hazitambuliwi kama mwahala tu zinakopita meli na vyombo vyengine vya majini, bali ni vitu vinavyoakisi historia, utambulisho na nguvu za taifa. Katika makala yetu ya juma hili tunaelekea kwenye Mlango-Bahari wa Hormuz; njia ya majini iliyotokea kwenye kitovu cha historia ya Iran, na ambayo leo hii inatajwa na kuzungumziwa zaidi duniani kuliko ilivyowahi kushuhudiwa katika wakati wowote ule huko nyuma.

Mlango-Bahari wa Hormuz ni njia muhimu ya baharini iliyoko kusini mwa Iran, ambayo tangu zama za kale imekuwa lango muhimu la mawasiliano ya baharini na biashara za kimataifa.
Njia hiyo ya majini sio tu inatambulika kuwa kiungo cha mawasiliano na biashara, lakini inajulikana pia kama alama na nembo ya umuhimu wa kijiografia na kihistoria wa Iran.
Mbali na umuhimu wake wa kiuchumi na kijeshi, Mlango-Bahari wa Hormuz una mvuto mkubwa pia wa kiutamaduni na kihistoria.
Miji, vijiji na bandari zinazouzunguka mlango huo wa bahari, zote ni wasimuliaji wa historia ya Wairani katika bahari na pwani, na namna ambavyo wamekuwa wakiamiliana na kushirikiana na majirani zao pamoja na ulimwengu kwa ujumla.

Jina “Hormuz” chimbuko lake linatokana na itikadi za kale za Wairani, na linarejea kwenye jina la mungu wao mkuu wa kale aitwaye Ahura Mazda. Tangu zama za Wasasani, jina hili lilikuwa likitumika kama jina takatifu linalotangulizwa kabla ya majina mengi yenye hadhi na itibari; na baada ya muda likaja kubadilika kuwa alama ya Mlango-Bahari wa Hormuz likiwa ni lango takatifu la Iran.
Kwa mtazamo wa kihistoria, kiuchumi na kijeshi, umuhimu wa Mlango-Bahari wa Hormuz ulishuhudiwa wazi katika enzi za Wahakhamanesh na Wasasani. Tafiti za wanaakiolojia zinaonyesha kuwa, katika zama za cha Wahakhamanesh, usimamizi wa Ghuba ya Uajemi ulikuwa ukifanyika kimfumo na kwa sura kamili; na Mkoa wa Ghuba ya Uajemi, ukiwa ndio kitovu cha mji wa Ufalme wa Wahakhamanesh wa Barazjan, yalikuwa ndio makao makuu ya kiidara, kisiasa na kibiashara ya eneo hilo.
Ilikuwa ni katika kipindi hicho pia, ambapo Dariush wa Kwanza wa Wahakhamanesh aliwahamishia Bahrain mabaharia wa Foinike ili kulibadilisha eneo hilo kuwa kambi ya kijeshi ya majini ya dola la Wahakhamanesh, kwa lengo la kulinda usalama wa Ghuba ya Uajemi.
Kwa kufanya hivyo, Wahakhamanesh waliweza kudhibiti safari za vyombo vya majini na biashara ya baharini katika Ghuba ya Uajemi, na kustawisha na kunawirisha njia mbalimbali za biashara.
Halikadhalika, ili kufanikisha mabadilishano ya kibiashara nje ya mipaka ya Ghuba ya Uajemi na kuingia kwenye bahari huru ya maji ya kimataifa, Wahakhamanesh waliunda kituo muhimu kilichojulikana kwa jina la “Makaa” au “Mokran” katika pande mbili za Mlango-Bahari wa Hormuz.
Kituo hicho muhimu kilikuwa na jukumu la kusimamia biashara ya baharini ya Iran kuelekea Bahari ya Hindi na Bara Hindi, huku Mlango-Bahari wa Hormuz ukiwa kitovu kikuu na muhimu cha njia hizo za kiuchumi.

Ghuba ya Uajemi ilikuwa sehemu ya eneo la jimbo la kumi na nne la dola la Wahakhamanesh, likijumuisha pia pwani za mkoa wa Hormuzgan, Oman na kusini mwa Sistan na Baluchistan ya leo.
Eneo hilo halikuwa makazi tu ya watu waliokuwa wakijihusisha na shughuli za baharini, lakini pia lilikuwa kituo kikuu cha usimamizi wa biashara ya majini ya Iran kutokea ardhi ya Pars kuelekea mashariki na Bara Hindi, ambapo wakati huo usalama na ulinzi kamili kwa ajili ya shughuli za kiuchumi katika Mlango-Bahari wa Hormuz vilikuwa vimeimarishwa kikamilifu.
Kadiri siku zilivyopita na kuanza zama za utawala wa Wasasani, ndivyo vituo vya kiidara na kibiashara vilivyohamishwa kutoka Mokran na kupelekwa Pars na katika mji wa Gur Firuzabad. Uhamishaji huo, sambamba na usimamizi makini wa bandari za kaskazini na kusini mwa Ghuba ya Uajemi, vilidhamini kuendelea kwa uhai wa kisiasa na kibiashara wa Iran katika eneo hilo.
Katika kipindi hicho, Mlango-Bahari wa Hormuz uliendelea kuwa kitovu cha biashara ya majini na mawasiliano ya kimataifa ya Iran, na ukaendelea kulinda nafasi yake kuu na muhimu katika usalama na utajiri wa taifa la Iran.
Katikati ya kipindi cha Wasasani, bandari za Rishahr na Najiram zilipata umuhimu mkubwa, na mwishoni mwa kipindi hicho, usimamizi wa Ghuba ya Uajemi ulihamishiwa katika bandari ya kihistoria ya Siraf.
Pamoja na hayo, Mlango-Bahari wa Hormuz uliendelea kuwa kitovu cha mawasiliano na biashara kati ya mashariki na Bahari ya Mediterania, huku Wairani wakidhibiti kikamilifu njia zake za baharini na za kiuchumi. 
Njia hiyo ya baharini haikuwa ya usafirishaji tu, lakini pia ilitambulika kama nembo ya mamlaka na nguvu za kitaifa za Iran.
Hata hivyo, ni vyema tukikumbushana tena kwamba, jina la Hormuz lina uhusiano wa tangu na tangu na itikadi na utamaduni wa Wairani.
Kwa kuchagua majina matakatifu kwa ajili ya maeneo muhimu ya kijiografia, Wairani wameonesha umuhimu wa kipekee wa Mlango-Bahari wa Hormuz kama nembo na alama ya umoja na mshikamano wa taifa lao. Jina hili limeendelea hadi leo kubaki kuwa lango takatifu la ardhi ya Iran na sehemu yenye umuhimu wa kimkakati katika eneo hilo.
Kwa hivyo, Mlango-Bahari wa Hormuz si njia tu ya baharini; bali ni nembo ya historia, utamaduni, usalama na utambulisho wa taifa la Iran.
Kutokana na usimamizi makini wa kisiasa, kiutawala na kijeshi uliokuwepo tangu zama za Wahakhamanesh hadi Wasasani, njia hiyo ya majini imekuwa na nafasi muhimu katika kuiunganisha Iran na ulimwengu, na umuhimu wake umeendelea kudumu hadi leo.

Kama tulivyotangulia kueleza, Wairani walikuwa wakichagua majina matakatifu kwa ajili ya maeneo muhimu ya kijiografia ya ardhi yao ili kuonyesha kwamba, hawayatazami maeneo hayo kama sehemu za kawaida tu zilizoko katika ramani, bali wanayafanya kuwa sehemu isiyotenganika na kumbukumbu zao za kihistoria, utambulisho wao wa kiutamaduni na hisia zao za uzalendo wa kitaifa.
Kwa mtazamo huo, umuhimu wa kipekee wa Mlango-Bahari wa Hormuz hauishii tu katika nafasi yake ya kimkakati au nafasi yake ya kiuchumi, bali umejikita pia katika fikra na utamaduni wa Wairani, na ni alama ya umoja, mshikamano na uhusiano wa kina wa ardhi hiyo na urithi wake wa kihistoria na kiroho.
Ukweli ni kwamba, pande zote nne za ardhi ya Iran zimethibitishwa kwa nyaraka na ushahidi madhubuti wa kihistoria; na kutambulishwa tena majina hayo katika muktadha wake wa kihistoria kunatoa taswira wadhiha na ya wazi kuhusu jiografia ya ustaarabu wa Iran.
Mfano wa majina hayo muhimu ya kihistoria ni mji wa Shush ulioko Khuzestan, ambao jina lake limetokana na mungu mkuu wa Elami aitwaye “Inshushinak”, na historia yake inarejea katika milenia ya tatu kabla ya kuzaliwa Nabii Isa AS, yaani takriban miaka elfu tano iliyopita.
Vilevile, jina la mji wa Yazd limetokana na neno “Izad”, lenye maana ya mungu mkuu katika imani za Wairani wa kale, ikiwa ni ishara ya kuendelea kudumu maisha ya kiutamaduni na kidini ya majina haya katika kipindi chote cha historia.
Ni vyema kukumbusha tena kwamba jina “Hormuz” chimbuko lake ni jina “Ahura Mazda”, mungu mkuu katika imani za Wairani wa kale; jina ambalo daima limekuwa likihusishwa na utakatifu na heshima katika historia na utamaduni wa Iran.
Kwa msingi huo, hatuwezi kuyachukulia maneno “Hormuz” na “Hormuzgan” kuwa ni majina tu ya kijiografia; bali ni mwangwi unaoakisi imani, utambulisho wa kiutamaduni na urithi wa kiroho wa watu wa Iran katika kipindi chote cha historia.
Ni kama alivyonukuliwa mtawala Dariush wa Wahakhamanesh katika maandishi yaliyosakafiwa kwenye athari za kale za magofu ya Persepolis akimsifu Ahura Mazda kwa kusema: “Mungu mkuu ni Ahura Mazda ambaye aliumba ardhi hii, akawaumbia watu furaha...”
Kwa hiyo, jina la Mlango-Bahari wa Hormuz, nalo pia ni kumbukumbu ya utamaduni huo wa kale wa kiimani na kihistoria; jina ambalo kwa Wairani si anwani ya kijiografia tu, bali ni sehemu ya kumbukumbu ya kihistoria na utambulisho wa taifa lao.
Historia fupi tuliyotoa mpenzi msikilizaji ya njia hiyo ya majini inakumbusha usimamizi erevu na makini wa Wairani katika uga wa usafiri wa baharini na biashara ya kimataifa; kuanzia kuhamishiwa Bahrain mabaharia wa Foinike, kuanzishwa vituo vya Mokran kwa ajili ya shughuli za mabadilishano ya kiuchumi, hadi usimamizi wa bandari muhimu katika zama za Wasasani.
Kwa mtazamo wa Iran, Mlango-Bahari wa Hormuz si kadhia ya kijiopolitiki tu; hiyo ni sehemu ya kumbukumbu ya kihistoria ya taifa ambalo kwa karne kadhaa limeelewa umuhimu wa bahari, biashara na mafungamano ya kimataifa, na limeweka mipango na mikakati madhubuti ya kuilinda njia hiyo ya majini.
Huenda dunia ya leo ikautambua Mlango-Bahari Hormuz kama njia kuu ya nishati, zaidi ya ilivyokuwa ikiutazama huko nyuma, lakini kwa upande wa Iran, ingali inaichukulia Hormuz kuwa ni kitu kikubwa zaidi ya kivuko cha majini; ni alama ya mamlaka na nguvu za kitaifa, utambulisho wa kihistoria na mahala panapoonyesha kuwa, baadhi ya sehemu za kijiografia si maeneo ya ardhi tu, bali ni kitu kinachohusu hatima ya mataifa.
Na maelezo hayo mpenzi msikilizaji, ndiyo yanayotamatisha makala yetu ya wiki kwa juma hili. Nakushukuru kwa kunisikiliza, na nakuombea kila lenye kheri na baraka maishani…/