Iran yataka kutokomezwa mfumo wa apartheid Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i100092-iran_yataka_kutokomezwa_mfumo_wa_apartheid_palestina
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametoa mwito kwa jamii ya kimataifa kusambaratisha mfumo wa ubaguzi wa rangi (apartheid) kote duniani na hususan huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Jul 19, 2023 09:15 UTC
  • Iran yataka kutokomezwa mfumo wa apartheid Palestina

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametoa mwito kwa jamii ya kimataifa kusambaratisha mfumo wa ubaguzi wa rangi (apartheid) kote duniani na hususan huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Nasser Kan'ani amesema hayo katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamiii wa Twitter kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela, kiongozi wa zamani wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini iliyoadhimishwa jana.

Tarehe 18 Julai kila mwaka huadhimishwa duniani kama Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela. Kampeni ya siku ya Mandela mwaka huu 2023 inamulika haki kwa wafungwa ikipewa jina #PrisonersMatter.

Kan'ani amesema wamimwengu hii leo wanahitaji fikra za kikombozi za rais wa zamani wa Afrika Kusini hayati Nelson Mandela, katika jitihada zao za kukabiliana na ubaguzi wa rangi katika pembe zote za dunia hasa Palestina.

Amekumbusha kuwa, Marekani iliunga mkono mfumo wa ubaguzi wa rangi wa apartheid nchini Afrika Kusini, na kwa msingi huo haina haki ya kujinadi kuwa mtetezi wa haki na demokrasia.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu (kulia) alipokutana na hayati Mandela huko nyuma

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amemtaja Mandela kama shujaa wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini na kote duniani, na pia rafiki wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.

Afrika Kusini ilitawaliwa na mfumo wa ubaguzi wa rangi wa apartheid kwa miaka 46, kuanzia mwaka 1948 hadi 1994, ambapo Mzee Mandela alisimama kidete kupinga jinai na ukandamizaji wa utawala wa makaburu nchini humo.

Aidha utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukiwakandamiza Wapalestina kwa kutumia sera zake za kibaguzi za apartheid tokea mwaka 1948, mkabala wa kimya cha jamii ya kimataifa.