Iran yazindua droni ya 'Mohajir-10' inayoruka kwa saa 24
(last modified Wed, 23 Aug 2023 02:38:01 GMT )
Aug 23, 2023 02:38 UTC
  • Iran yazindua droni ya 'Mohajir-10' inayoruka kwa saa 24

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imezindua ndege isiyo na rubani yenye uwezo wa kuruka kwa saa 24 mfululizo bila kusimama.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, droni hiyo iliyozunduliwa jana Jumanne imepewa jina la 'Mohajir-10' na ina uwezo wa kioperesheni wa kilomita 2,000.

Ndege hiyo isiyo na rubani iliyoundwa na wataalamu wa hapa nchini, imezinduliwa kwa mnasaba wa Siku ya Viwanda vya Zana za Ulinzi vya Iran iliyoadhimishwa jana Jumanne.

Droni ya Mohajir-10 mbali na kuwa na uwezo wa kujazwa mafuta hadi lita 450, lakini pia inaweza kuruka kwa kasi ya kilomita 210 kwa saa. Kadhalika ina uwezo wa kubeba aina mbalimbali ya mabomu na maroketi.

Hali kadhalika, droni ya Mohajir-10 iliyozinduliwa jana hapa nchini imeshehenezwa kwa mifumo ya vita vya kielektroniki na mifumo ya kukusanya taarifa za kiitelijensia.

Rais wa Iran katika maonyesho ya zana za kijeshi na kiulinzi za Jamhuri ya Kiislamu mjini Tehran

Akizungumza pambizoni mwa hafla ya kuzinduliwa droni hiyo, Rais Ebrahim Raisi wa Iran ameagiza kuanza mchakato wa kukabidhiwa Majeshi ya Ulinzi ya Iran na Kikosi cha Anga za Mbali cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) makombora ya “Khorramshahr” na “Haj Qassem”. 

Aidha hapo jana, Mkuu wa Komandi Kuu ya Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Meja Jeneral Mohammad Baqeri alisema nguvu za kiulinzi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zilizoko katika nyuga tofauti, zinathibitisha ubunifu wa kila namna wa kupigiwa mfano wa taifa hili kiasi kwamba hata madola makubwa ya kijeshi ulimwenguni yameonesha hamu ya kustafidi na mafanikio hayo ya Iran.