Mahudhurio ya Rais Raisi katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
Rais sayyid Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa mara pili akiwa kiongozi wa serikali, ameelekea nchini Marekani kuhutubia kikao cha 78 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Ajenda kuu ya safari hiyo ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ni kuhutubia Bazara Kuu la Umoja wa Mataifa, kuonana na kuzungumza na viongozi wa nchi mbalimbali pamoja na kufanya mazungumzo na Wairani wanaoishi nchini Marekani. Katika vikao yake mbalimbali na makundi ya kibinafsi ya kisiasa, kijamii, kidini na vyombo vya habari vya Marekani, Rais Ebrahim Raisi atajibu maswali na kuweka wazi misimamo na mitazamo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusiana na masuala mbalimbali ya kieneo na kimataifa.
Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hufanyika kila mwaka kuanzia wiki ya tatu ya mwezi Septemba kwa hotuba za viongozi wa kisiasa na marais wa nchi mbalimbali duniani. Katika hotuba yake ya kwanza Septemba mwaka jana kwenye baraza hilo, Sayyid Ebrahim Raisi aliashiria jinai iliyofanywa na Marekani ya kuunda na kuunga mkono kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) vilevile amri ya Donald Trump ya kuuliwa shahidi Jenerali Haj Qassem Soleimani kisha akainua juu picha yake na kukaa kimya kwa dakika chache. Raisi pia alisisitiza ulazima wa pande zote kuheshimu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na maazimio ya Umoja wa Mataifa na kusema kwamba, serikali yake inafuatilia sera za kuwa na uhusiano mwema na nchi zote za ulimwengu, hasa nchi jirani.

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ni moja ya nguzo kuu tano za jumuia hiyo ya kimataifa na nguzo pekee ya Umoja wa Mataifa ambamo wanachama wote wana haki sawa ya kupiga kura. Kwa sababu hiyo, safari ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini New York ikapewa muhimu maalumu. Hii ni kwa sababu, safari hiyo inahesabiwa kuwa ni fursa kwa Iran kutoa maoni yake kuhusiana na matukio muhimu ya kimataifa. Kuhudhuria kila mwaka viongozi wengi wa ngazi za juu wa kisisa wa nchi mbalimbali katika vikao vya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa huandaa fursa nzuri ya kufanyika mashauriano muhimu ya pande mbili na katika ngazi za kisiasa duniani.
Rais wa Iran pia alisema sababu ya kuhudhuria kwake kikao hicho ni kubainisha na kuweka wazi mitazamo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuongeza kuwa: "Mkutano wa Umoja wa Mataifa ni uwanja wa kubainishwa mitazamo na sera za Iran, mitazamo ambayo lengo lake ni kuwepo ulimwengu usio na umaskini, silaha za nyuklia, mauaji ya umati, dhuluma na ubaguzi; ulimwengu ambamo ubinadamu utazingatiwa kupelekwa uwezo wake unatumika kuzuia majanga mbalimbali ya kimaumbile yanayosababishwa na sera na siasa za kujitanua.
Nukta nyingine muhimu kuhusiana safari ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Irani huko New York ni kuwa, unafanyika katika hali ambayo Iran, katika kipindi cha mwaka moja uliopita, imeweza kufungua ukrasa mpya wa kidiplomasia na vilevile kuandaa uwanja wa mashauriano na nchi nyingine na jumuia za kieneo na kimataifa. Katika kipindi hiki pia Tehran imepata uwanachama katika jumuia za Shanghai na BRICS pamoja na kuboresha na kuimarisha uhusiano wake na nchi jirani kwa kadiri kwamba, baada ya kuboreka uhusiano wa Tehran na Riyadh, baadhi ya nchi zilizokuwa na uadui na Jamhuri ya Kiislamu pia hivi sasa zinaomba kuimarisha ushirikiano wa pande mbili.

Wakati huo huo, Iran na Marekani ziko katika mchakato wa mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na ya hatua kwa hatua, ili kwamba iwapo Marekani itaheshimu ahadi na wajibu wake wote, kuweze kutazamwa uwezekano wa kuanzishwa mazungumzo ya kuondoa vikwazo. Kwa hivyo, kwa kutilia maanani kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikionyesha ushirikiano wa hali ya juu katika mchakato wa mazungumzo, vikao vya Raisi kando ya Mkutano wa Baraza Kuu la UN vinaweza kuwa fursa ya kuzihimiza nchi zote kuunga mkono mchakato wa mazungumzo hayo.
Nasser Kan'ani, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuhusiana na suala hilo kuwa, kuna uwezekano wa kuendeleza mazungumzo ya kuondolewa vikwazo pembezoni mwa mkutano wa Umoja wa Mataifa.
Kwa msingi huo, uwepo wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kunatambuliwa kuwa ni fursa mpya ya kuakisi misimamo na mitazamo ya Jamhuri ya Kiislamu na kufanya mashauriano ya kidiplomasia yatakayoanda uwanja kwa ajili ya kutekelezwa sera na malengo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.