Rais wa Iran: Kubadilishana wafungwa na Marekani ni hatua ya kibinadamu pekee
(last modified Tue, 19 Sep 2023 13:52:03 GMT )
Sep 19, 2023 13:52 UTC
  • Rais Ebrahim Raisi
    Rais Ebrahim Raisi

Rais Ebrahim Raisi wa Iran anasema mabadilishano ya wafungwa yaliyofanyika kati ya Iran na Marekani yalifanywa kwa misingi ya kibinadamu tu.

Raisi, ambaye yuko New York kushiriki katika Mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na wasimamizi wakuu wa vyombo vya habari vya Marekani jana Jumatatu baada ya Iran na Marekani kutekeleza makubaliano ya kubadilishana wafungwa yaliyosimamiwa na Qatar.

Akibainisha kwamba kubadilishana wafungwa kati ya Iran na Marekani ni hatua ya kibinadamu tu, Rais wa Iran alisema, "Bila shaka, hatua yoyote itakayochukuliwa [na Marekani] kutimiza ahadi zake itakuwa ni kujenga imani kwetu."

Raisi ameiambia televisheni ya NBC kwamba fedha zilizotolewa, ambazo amesema zimezuiwa kikatili na sasa zinamilikiwa na Iran, ni za watu wa Iran na zitatumika kukidhi mahitaji yao.

Baada ya miaka miwili ya mazungumzo ya hali ya juu, Iran na Marekani zilikubali kuwaachia huru wafungwa wa pande mbili kama sehemu ya makubaliano ambayo pia yalijumuisha kuachiliwa kwa mabilioni ya fedha za Iran zilizoshikiliwa kinyume cha sheria nchini Korea Kusini.

Fedha hizo za Iran zilizotokana na mauzo ya nje ya mafuta na gesi, zilikuwa zimefungiwa katika akaunti za benki za Korea Kusini tangu mwaka 2018 baada ya utawala wa rais wa wakati huo Donald Trump kuiondoa Marekani kwenye mkataba wa kihistoria wa nyuklia na Iran, na hivyo kuzidisha mvutano kati yake na Tehran.

Siku ya Jumatatu, Iran na Marekani ziliwaachilia huru wafungwa 10 -- Wairani watano na Wamarekani watano -- baada ya serikali ya Washington kuruhusu uhamisho wa dola bilioni 6 za fedha za mafuta ya Iran zilizokuwa zimezuiliwa nchini Korea Kusini.

Ndege iliyowabeba Wairani wawili kati ya watano walioachiliwa ilitua Tehran Jumatatu jioni. Mehrdad Moein Ansari na Reza Sarhangpour waliwasili Tehran wakitokea Doha nchini Qatar mapema jana asubuhi.

Wairani wengine watatu walioachiliwa huru hawajarejea Iran, huku wawili wakibaki Marekani na mmoja kwenda nchi ya tatu kujiunga na familia yake.

Wafungwa watano wa Kimarekani, ambao walitolewa nje ya Iran mapema Jumatatu kama sehemu ya makubaliano ya kubadilishana wafungwa, pia waliondoka na msuluhishi wa Qatar kwenda Marekani.