Sep 25, 2023 03:12 UTC
  • Raisi: Iran haina mpango wa kumiliki silaha za nyuklia

Rais wa Iran amepuuzilia mbali madai ya madola ya Magharibi kwamba Jamhuri ya Kiislamu inataka kuunda silaha za nyuklia.

Sayyid Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema hayo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya CNN ya Marekani pambizoni mwa Mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York na kusisitiza kuwa, Iran haina nia kabisa ya kuunda au kumiliki silaha hizo za maangamizi ya umati.

Aidha ametetea hatua ya urutubishaji wa madini ya urani nchini kwa kiwango cha asilimia 60 kwa mujibu wa sheria iliyopitishwa na Majlisi (bunge) mwezi Disemba 2020 na kubainisha kuwa, sheria hiyo inataka kuharakishwa maendeleo ya mpango wa nyuklia wa Iran wenye malengo ya amani.

Rais wa Iran amesema sheria hiyo iliyopewa jina la Mpango wa Mkakati wa Kukabiliana na Vikwazo na unaolenga kukabiliana na vikwazo na kuendeleza mpango wa amani wa nyuklia wa Iran, ilipasishwa baada ya Ulaya kushindwa kufungamana na majukumu yake kwenye mapatano ya JCPOA.

Rais wa Iran katika Mkutano wa 78 wa UNGA

Sayyid Raisi ameeleza bayana kuwa, Jamhuri ya Kiislamu imeazimia kikweli kuendeleza mpango wake wa amani wa nyuklia na kushirikiana na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kwa mujibu wa haki na wajibu ulio chini ya mpango huo. Wakala wa IAEA umesema mara chungu nzima kwenye ripoti zake kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haina ratiba zozote za kumiliki silaha za atomiki na kwamba mradi wake wa nyuklia ni wa amani kikamilifu. 

Aidha katika mahojiano hayo na mwandishi wa habari wa CNN, Fareed Zakaria, Rais wa Iran amesema jitihada za Marekani za kutaka mataifa ya Kiarabu ya Ghuba ya Uajemi ikiwemo Saudi Arabia kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel hazitafua dafu.

Tags