Sep 28, 2023 03:01 UTC

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu amesema: Makubaliano ya kieneo na ya kimataifa yaliyoundwa duniani chini ya usimamizi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yameibua matumaini katika nyoyo za Waislamu duniani.

Shirika la Habari la Iran (IRNA) limeripti kuwa, Hujjatul Islam Hamid Shahriyari, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu amesema katika mkutano na waandishi wa habari wa Kongamano la 37 la Kimataifa la Umoja wa Kiislamu mjini Tehran kwamba: Kutokana na juhudi zake katika uga wa kimataifa, Serikali ya Awamu ya 13 ya Iran imekuja na tunu ya kuzidisha ushirikiano wa karibu baina ya nchi za Kiislamu na Iran, na ushirikiano huo unaojumuisha usalama wa kikanda.

Shahriyari amesema: Kuwa na ushirikiano na washirika na kushikamana na maagano na ahadi ni masuala mawili ambayo yameagizwa katika Qur'ani Tukufu; na nchi za Kiislamu zinaweza kuelekea kwenye umma mmoja kwa kushikamana na maagano na ahadi.

Kongamano la 37 la Kimataifa la Umoja wa Kiislamu litafanyika mjini Tehran kwa anwani ya "Ushirikiano wa Kiislamu kwa Lengo la Kufikia Maadili ya Pamoja" kuanzia tarehe 1 hadi 3 Oktoba, na kupitia jukwaa la mtandao kuanzia leo Alkhamisi hadi tarehe 3 Oktoba.

Ni vyema kukumbusha hapa kuwa, leo Alhamisi, tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul-Awwal 1445, kwa mujibu wa nukuu za baadhi ya wanahistoria, ni siku ya kumbukumbu ya Maulidi na kuzaliwa Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu, Muhammad al Mustafa (SAW), na mwanzo wa Wiki ya Umoja baina ya Waislamu.

Maadhimisho ya Maulidi ya Mtume (SAW) nchini Yemen

Waislamu wa madhebu za Suni huadhimisha siku hiyo tarehe 12 Rabiul Awwal, huku wenzao wa madhebeu ya Shia wakiadhimisha Maulidi na siku ya kuzaliwa mbora huyo wa viumbe tarehe 17 mwezi huu wa Rabiul Awwal. 

Kipindi hiki cha baina ya tarehe 12 na 17 Mfunguo Sita kimetangazwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa ni Wiki ya Umoja na Mshikamano Baina ya Waislamu wote duniani, lengo likiwa ni kuwakusanya pamoja Waislamu wote wa madhehebu na mitazamo tofauti katika Tauhidi na umoja wa Kiislamu. 

Tags