Raisi aitaka jamii ya kimataifa isimamishe jinai za Israel Ukanda Gaza
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameikumbusha jamii ya kimataifa kuwa ina wajibu wa kukomesha mgogoro katika wa Ukanda wa Gaza, ambapo Wapalestina wa eneo hilo wanakabililiwa na kila aina ya jinai kutoka kwa Wazayuni.
Akihubutia kikao cha Baraza la Mawaziri jana Jumatano hapa Tehran, Rais Ebrahim Raisi wa Iran amelaani vikali jinai zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina katika Ukanda wa Gaza.
Amesema, "Wazayuni wanafanya jinai dhidi ya binadamu mbele ya macho ya dunia. Taasisi na mashirika yote ya kimataifa yanapaswa kutekeleza jukumu lao kuhusiana na hili pasi na ubaguzi."
Kadhalika Rais wa Iran amekosoa vikali hatua ya baadhi ya mataifa ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel na kufanya mapatano na utawala huo ghasibu.
Aidha Sayyid Ebrahim Raisi ameyataka mataifa ya Kiislamu na umma wote wa Kiislamu kuwaunga mkono kwa dhati wananchi madhulumu wa Palestina.
Kwa siku ya sita mfululizo, utawala wa Kizayuni wa Israel umeendelea kuushambulia Ukanda wa Gaza kwa makombora, ambapo Wapalestina zaidi ya 1,055 wameuawa shahidi.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameitaka jamii ya kimataifa ichukue hatua za dharura za kukomesha jinai hizo za kuogofya za utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda Gaza.