Nov 23, 2023 07:35 UTC
  • Raisi: Israel haijaambulia chochote katika vita vyake Gaza

Rais Ebrahim Raisi wa Iran amesema Israel imefeli kufikia malengo yake yote katika hujuma na mashambulizi yake ya kinyama dhidi ya wananchi wa Palestina katika Ukanda wa Gaza.

Rais Raisi alisema hayo jana Jumatano hapa Tehran katika mahojiano na wanahabari wa kanali tano za televisheni zinazotangaza kwa lugha ya Kiarabu na kubainisha kuwa: Israel haikufikia hata moja ya malengo yake, ama kuikalia kwa mabavu Gaza au kuusambaratisha muqawama.

Sayyid Raisi alifanyiwa mahojiano hayo na stesheni ya televisheni ya al-Manar ya Lebanon, al-Etejah ya Iraq, al-Aqsa TV na Palestina Today za Palestina, na al-Masira ya Yemen.

Rais wa Iran ameshiria vita vya Israel dhidi ya Wapalestina wa Gaza na kueleza bayana kuwa: Kile ambacho utawala wa Kizayuni umefanya, kimefichua namna (utawala huo) ulivyoshindwa na kukata tamaa, mkabala wa muqawama wa Palestina.

Kadhalika ameitaja Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa kama jibu halali la taifa la Palestina, mkabala wa dhulma za muda mrefu za utawala ghasibu wa Israel.

Kimbunga cha al-Aqsa kimetoa kipigo kwa Israel na washirika wake

"Taifa, ambalo makazi yake yameghusubiwa, jamaa zake ama wamefungwa jela au kuuawa shahidi, na ambalo mashamba yake yameharibiwa, lina haki halali ya kujilinda kwa kutumia viwango vyovyote vyenye mantiki," ameongeza Sayyid Raisi.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha kuwa, operesheni ya Wapalestina imeusababishia utawala wa Kizayuni hasara na pigo la kijeshi, kiusalama na kiintelijensia. 

Aidha amegusia kuhusu kitendo cha Wazayuni kuwaua shahidi Wapalestina zaidi ya 14,500 mpaka sasa katika mashambulizi yake ya kikatili dhidi ya Gaza tokea Oktoba 7 na kusisitiza kuwa, "Kuua wanawake na watoto sio ushindi. Mauaji ya halaiki ya watoto na wanawake yameibua anga ya chuki ambayo haijawahi kushuhudiwa dhidi ya Israel kote duniani."

Tags